Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 30 May 2013

Wabunge kupokea dola 10,000 kwa mwezi Kenya

Tume ya  kitaifa ya mishahara imekana vikali malipo hayo ya wabunge ambao wanayataka
Nairobi. Tume ya Taifa ya kuratibu mishahara ya maofisa wa serikali (SRC) imesema kuwa makarani wa bunge huenda wakaingia matatani kwa matumizi mabaya ya ofisi na fedha za umma iwapo watakubali kuongeza mishahara ya wabunge.
Mwenyekiti wa SRC Sarah Serem alimuonya karani wa Bunge la Kitaifa, Justin Bundi na mwenzake wa Seneti, Jeremeiah Nyegenye kuwa watawajibika kwa matumizi mabaya ya ofisi na fedha za umma kama watawalipa wabunge mishahara zaidi ya kiwango kilichotangazwa.
“Katiba inatupa mamlaka ya kuratibu mishahara ya maafisa wa serikali. Na hivyo ndivyo tulivyofanya,’’ alisema mwenyekiti wa tume hiyo Serem.
Serem alisema kuwa tume hiyo ilichapisha mishahara watakayopokea wabunge kwenye gazeti rasmi la serikali kwa nia nzuri.
Licha ya wananchi wa Kenya kuandamana mpaka nje ya Bunge, wiki mbili zilizopita wabunge nchini humo wameamua kujipigia kura ya kujiongezea mishahara.
Wabunge hao wameenda kinyume na Tume ya Kitaifa ya kuratibitisha mishahara ya maofisa wa serikali (SRC).
Juzi wabunge hao walipiga kura hiyo wakiwa bungeni ambapo sasa wanaweza kupokea kitita cha Dola 10,000 kwa mwezi.
Rais Uhuru Kenyatta aliwaomba wabunge hao mapema mwezi huu kuruhusu mishahara yao kupunguzwa ili waweze kuiwezesha serikali kupata pesa za kutengeneza ajira kwa wananchi.
Kutokana na kiasi hicho ambacho wabunge wamekiidhinisha kinadhihirisha kwamba wao ndio wanaopokea mishahara mikubwa Afrika.
Wabunge hao hawakutaka kusikiliza vilio vya wananchi wao ambao waliandamana kwa lengo la kupinga ongezeko hilo kubwa la mshahara.
Wananchi kwa ghadhabu waliamua kufanya maandamano huku wakiwafananisha wabunge hao  na nguruwe kwa ulafi.

0 comments:

Post a Comment