Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 23 May 2013

Vurugu Mtwara TZ; Rais Kikwete atoa tamko kali

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amekemea vikali vurugu zilizotokea jana mkoani Mtwara kusini mashariki mwa nchi hiyo baada ya kusomwa bungeni kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Akizungumza mjini Dodoma, Rais Kikwete amesema wote waliohusika na vurugu hizo watasakwa na kuchukuliwa hatua kali. Aliongeza kuwa rasilimali inayopatikana mahali popote pale nchini inatakiwa kutumiwa na Watanzania wote. Akizungumza bungeni jana Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema mradi wa kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam, umeanza kwa kasi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atakwenda huko wiki ijayo kuweka jiwe la msingi. Tamko hili la Muhongo ndilo lililoibua vurugu kubwa Mtwara. Aidha jambo lingine linalosemekana limesababisha ghasia hizo ni hatua ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutokurusha moja kwa moja matangazo ya Bunge hivyo kuwakosesha wananchi fursa ya kusikiliza bajeti hiyo. Baadhi ya duru zinasema mtu mmoja amefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na vurugu hizo. Milio ya risasi za moto na mabomu ya machozi vilisikika katika maeneo kadhaa ya Mtwara ambako hali ilikuwa mbaya kutokana na kuzuka mapambano kati ya polisi na vijana waliokuwa na hasira.

0 comments:

Post a Comment