Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Monday 20 May 2013

UDINI: Tuambizane ukweli, hivi tatizo ni mihadhara?

 
HAPO kitambo kidogo niliandika makala katika gazeti la Raia Mwema nikiomba waumini wote wa kiislamu na kikristo ‘wachinje’ imani zao ili Taifa libakie salama. Naona makala ile haikueleweka kwani baada ya tukio la hivi karibuni la kulipuliwa kanisa huko Arusha sasa wamejitokeza watu na hasa viongozi wa kidini na wa kisiasa wakidai mihadhara ya wazi ipigwe marufuku kana kwamba mihadhara ndio sababu kuu ya watu kumwagiana tindikali, kulipuana kwa mabomu, kugombea kuchinja, kuchinjana na kupigana risasi!
Napenda awali ya yote niseme kuwa mie ni mmoja wa waliokerwa sana pale Taifa lilipoanza kuruhusu mihadhara hadi hata kufikia kuwaruhusu waumini wa dini mbalimbali kuanzisha ‘mashindano’ ya kutumia viwanja vya michezo na sehemu nyingine za umma kwa mahubiri. Na viongozi wetu wa serikali wakawa wageni mashuhuri kwenye mihadhara hiyo! Nao sasa wanapiga kelele ‘mihadhara ifutwe’!
Kwa wale wa umri wangu watakumbuka kwamba kabla ya ujio wa utawala wa Mzee Mwinyi mihadhara ilikuwa inafanywa na waumini wa kikristo hasa pale Jangwani, mjini Dar es Salaam. Nyakati hizo tulishuhudia ujio wa wahubiri wa kikristo toka nchi mbalimbali. Hizi zilikuwa zile enzi za November Crusades’ pale Jangwani.
Lazima tukiri kwamba; kama ni dhambi ya mihadhara, basi, ilianza kabla ya utawala wa Mzee Mwinyi, na washiriki wakubwa walikuwa wahubiri wa dini ya kikristo. Lakini lazima pia tukiri nyakati hizo kebehi na matusi dhidi ya imani nyingine nayo haikuwa kubwa ingawaje kulikuwa na malalamiko hapa na pale kutoka kwa waislamu. Waislamu nao wakadai wapatiwe fursa ya kufanya mihadhara maeneo ya wazi.
Kwa vijana wa siku hizi na wale ambao wanajifanya wamesahau, wakumbuke kuwa toka miaka ya mwanzoni mwa uhuru hadi miaka ya 70 ilikuwa si rahisi kwa waumini wa kiislamu kupata kibali cha kuendesha mihadhara kama tuliyoishuhudia kuanzia miaka ya themanini.
Ikumbukwe kuwa kwa miaka mingi tu waislamu hawakuwa na TV, gazeti wala redio, na hata pale walipotaka kuanzisha mambo hayakuwa rahisi sana kwao.
Nimeelezea hili ili tukumbuke ni kina nani hasa walianzisha hili suala la mihadhara. Kabla ya utawala wa Mzee Mwinyi mihadhara pekee ya dini ya kiislamu ilikuwa ni siku ya Maulidi.
Mihadhara hii ilikuwa inafanyika usiku sehemu nyingi na ilikuwa inatawaliwa na masuala ya kiimani na ilikuwa nadra kusikia kashfa dhidi ya dini nyingine. Kwa kumbukumbuku yangu, sikuwahi kusikia malalamiko toka kwa ndugu zetu wa kikristo dhidi ya mihadhara ya Maulidi.
Kwa hakika, malalamiko dhidi ya mihadhara ya Maulid yalikuwa miongoni mwa wasilamu wenyewe, baadhi wakikubali uwepo wa Maulid wengine wakidai Maulid ni bidaa!
Lakini dhambi ya kuruhusu mihadhara ya nje ya nyumba za ibada ilianza kututafuna pale ambapo waislamu nao walipoanza kuendesha mihadhara ya viwanjani, redioni, kwenye TV na magazeti.
Mara ghafla kukawa na ‘mashindano’ ya kuendesha mihadhara na aina nyingine ya mahubiri nje ya nyumba za ibada. Ikaanza kuwa mazoea ukienda sokoni au ukipita barabarani unakuta mtu anahubiri hadi sauti inamkauka!
Kukazuka vikundi vinapita majumbani mwa watu eti kutoa neno hata kama mwenye nyumba au chumba si wa imani yao! Ukipita barabarani unapewa kwa njia ya kulazimisha gazeti, maandiko au vitabu vya imani isiyokuwa yako!
Ukiingia kwenye basi yupo mhubiri! Anahubiria hata wasio wa imani yake eti kwa kuwa tu mwenye chombo cha usafiri naye anaona ndio mchango wake kwa kumruhusu mhubiri yule ahubiri!
Ndani ya mabasi ya abiria ambao ni wa imani tofauti tukaruhusu kanda na sinema za imani fulani zionyeshwe! Akitokea abiria wa imani tofauti aseme kanda au video izimwe inakuwa mtafaruku! Matendo haya yakitendwa zaidi na waumini wa dini za kikristo.
Waislamu nao tukaanza kuona vikundi vya mahubiri (wao wanaita daawa). Vikundi hivi vikawa kashfa dhidi ya wakristo (wao wakiwaita Wagalatia) mtindo mmoja! Vikundi hivi vikawa na vyombo vya kisasa kabisa na vikaanza kuzunguka nchi nzima vikitoa kashfa dhidi ya wakristo!
Kanda zikaandaliwa za kashfa tupu! Hujifunzi lolote la maana katika imani ya kiislamu zaidi ya kwamba Yesu si Mungu na ‘uongo’ wa Mtume Paulo! Mafundisho namna ya kusali, kufunga, nk. wao hapana; bali kashfa tu!
Baadhi ya vikundi vya kikristo navyo vikaingia mtegoni; maana vilikubali kuandaa mihadhara ya pamoja ili kuonyeshana ufundi wa kukashifu imani ya wenzako! Mihadhara hii ya pamoja ikarekodiwa na kanda zikasambazwa ndani na nje ya nchi!
Kwa vijana na watoto, hizi kanda ndo zikawa kama vitabu rejea vya wanafunzi mashuleni! Mihadhara ikawa ndio ‘lecture theatres’ zao! Sasa watoto wanakojolea quran eti tunashangaa!
Kama nilivyoeleza hapo juu, ni kweli mihadhara imechangia kwa kiasi fulani katika mgawanyiko huu wa Taifa, lakini je; mihadhara ndio kianzilishi (cause)?
Kwa wale waliochoka kufikiri au wale wasioitakia mema nchi yetu, jibu lao litakuwa ‘ndio’! Lakini kwa wale wanaousumbua bongo zao kufikiri, wazalendo na wenye nia njema na nchi yetu na watu wake, jibu ni ‘hapana’.
Mihadhara, mabomu, tindikali, ugomvi wa kuchinja, kuchinjana na kupigana risasi ni dalili (symptoms) za ugonjwa. Taifa ‘linaumwa’ lakini kwa bahati mbaya ‘madaktari’ wake wanakimbilia kuumwagia maji mwili wake eti kwa kuwa joto limepanda sana!
Ni kama kujaribu kumaliza malaria kwa kufunga bandeji kichwani au kwa kununua klorokwini kwa wingi! Mgonjwa hatapona, atakufa tu! Tunapaswa si kuangamiza mbu pekee bali kuangamiza mazingira yanayosababisha mbu kuzaliana.
Labda nijaribu kuelezea sababu zinazolifanya Taifa liwe gonjwa. Najua wengine wengi wameshagusia mambo haya, lakini kwa kuwa ‘madaktari’ bado hawajazinduka, inapaswa tuendelee kukumbushana ili siku moja wote tusiathirike. Au majaaliwa ya Mungu siku moja madaktari wazinduke na kutupatia tiba muafaka.
Na katika kukumbushia, tunatakikana tusimwonee yeyote haya; maana hata kama ni wa imani yako, anaweza kukudhuru!
Siasa za majitaka
Siasa za majitaka ambazo hata mmoja wa viongozi wa CCM alipokuwa anajiuzulu alithibitisha ndio dira kuu ya chama hicho, ndio chanzo kikuu cha mgawanyiko tulionao. Ukitaka kujua CCM imedumbukia kwenye siasa majitaka rejea yafuatayo:
  • Ilani ya uchaguzi ilipowahakikishia waislamu Mahakama ya Kadhi.
Binafsi naamini bila kuwapatia waislamu Mahakama ya Kadhi tutaendelea na misuguano isiyo lazima. Katika makala zangu za awali nimeshaeleza udhaifu wa hoja kwamba hili ni suala la imani lisigharamiwe na serikali.
Tuna masuala mengi ya kiimani ambayo yanagharamiwa na serikali ikiwa ni pamoja na misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini, huduma kwa ubalozi wa Vatican, n.k. Na huko hatusikii hoja hii ikijitokeza.
Pia naamini tunaikuza mno Mahakama ya Kadhi. Mimi naamini kutakuwepo hata baadhi ya waislamu wataopendelea kwenda mahakama za kawaida hata hiyo mahakama ikiwepo.
Huko nyuma ilipokuwepo ilikuwa hivyo.
Binafsi, naamini CCM ingeweza kuhakikisha Mahakama ya Kadhi inapatikana bila kuingiza kwenye ilani yake ya uchaguzi. Si CCM ndiyo ilikuwa na uhakika wa kuunda serikali?
Ubaya ulikuwa  ni kutumia hitajio la watu wa imani fulani ili kujipatia kura kwenye uchaguzi. Kitendo hiki ndicho kiliweka mstari wa kwanza wa kutenganisha Watanzania kwa msingi wa imani. Waliotayarisha, kuipitisha na kuighani ilani ile ndio tunaopaswa kuwawajibisha au kuwarekebisha kama tunataka kuwa salama.
Hawa hawakutoa mhadhara lakini dhambi yao ni kubwa kuliko ya watoa mihadhara.
Tukiwafumbia macho watarudia tena kama si kwenye uchaguzi wa 2015 itakuwa chaguzi nyingine. Si ndio mbinu iliyowapatia kura nyingi toka kwa waislamu?
  • Mbinu za kupata kura kwa kubambikiza kuwa baadhi ya vyama au viongozi wa vyama hivyo ni vya / wa dini fulani.
Kauli za wanasiasa hawa, hasa wa CCM, zilikuwa na madhara makubwa kuliko mihadhara wanayotaka kuipiga marufuku. Hawa wanaweza kuendeleza kauli hizo mwaka 2015 kwa kuwa wanaamini ndio njia ya kupata ushindi wa kishindo.
Kama ni kupiga marufuku, tunapaswa kwanza kuwapiga hawa marufuku kabla ya kupiga marufuku mihadhara. Tusipozinduka kwa hili tujiandae kwa vyama vya kisiasa vitakavyokuwa kwa misingi ya kidini huko tuendako.
Kama si vyama, basi, tujiandae watu kupiga kura kidini. Si tumeanza kuona dalili kwenye uchaguzi wa mabaraza ya katiba? Au tunajifanya hatuoni?
  • Uchaguzi wa Spika kwa msingi wa maumbile: ubaguzi wa aina moja huibua ubaguzi wa aina nyinginezo.
Huwezi kuwa na jamii (hasa viongozi) inayoruhusu ubaguzi wa aina moja halafu ukadhani ubaguzi huo utakomea hapo. Hii ndio falsafa ya ubaguzi; ubaguzi hausimami peke yake.
Walioanza kutuelekeza tutizamane kwa maumbile ndio waliopandikiza ubaguzi wa aina nyingine. Ni kama ubaguzi umeruhusiwa rasmi! Itakuwa vipi uchaguzi ujao wa Spika waislamu wakasema kwa kuwa maspika wengi waliotangulia walikuwa wakristo sasa ni zamu ya waislamu kutoa spika? Si hao wanasiasa wa maji taka wametuonyesha kuwa badala ya kuangalia viwango tunaweza kuangaliana kimaumbile, kidini, kikabila nk?
  • Uendeshaji wa bunge na lugha zinazotolewa ndani ya bungeni moja ya aina mbaya ya siasa za majitaka.
Kwa jinsi uongozi wa bunge unavyoachia lugha za matusi zivurumishwe, hasa na wabunge wa CCM, ipo siku lugha ya matusi haitakuwa dhidi ya wabunge wa upinzani bali itakuwa dhidi ya imani ya kidini ya watu fulani au dhidi ya hoja iliyotolewa na wabunge wa upinzani ambayo itakuwa inatetea maslahi ya waumini wa dini fulani. Nchi italipuka!
Wanaoendeleza mzaha huu pale bungeni lazima waelewe ipo siku wataitumbukiza nchi kwenye matatizo makubwa ya kidini.
Kukosekana kwa haki
Haki ya mtu au kikundi cha watu ni pamoja na kusikilizwa hata kama madai yao hayana hoja. Kwa miaka nenda rudi waislamu wamekuwa wakitoa malalamiko kuhusu wasivyoridhishwa na BAKWATA, uwiano wa wanafunzi kwenye taasisi za elimu, uwiano wa watumishi serikalini, kufutwa kwa Mahakama ya Kadhi, nk.
Badala ya hoja hizi kusikilizwa na kutolewa ufafanuzi au kutafutiwa ufumbuzi, serikali imekuwa aidha ikikaa kimya au kutoa kauli tata au kuwaachia viongozi wa dini nyingine kujibu malalamiko ambayo hawakupelekewa wao. Utadhani maaskofu ndio wamekuwa wasemaji wa serikali!
Baadhi ya waislamu kwa kukosa majibu murua toka kwa serikali, na kwa kuchukizwa na majibu yanayotolewa na viongozi wa dini ambao hawakuwapelekea matatizo yao, wameamua kuonyesha hasira zao kwa njia mbalimbali.
Ili tuwe salama, inapaswa Serikali itoke na kuzungumza na waislamu kuhusu malalamiko yao. Kwa mfano kama BAKWATA inalalamikiwa kwa nini Serikali kama ilivyoshughulikia uundwaji wa BAKWATA, isisimamie mchakato wa kuunda chombo kitakachokubalika na waislamu kama sio wote, basi, wengi wao?
Hivi hatuoni kuwa na chombo ambacho tunajidanganya ndicho kinasimamia maslahi ya waislamu wote; ilhali kinapingwa na idadi kubwa ya waislamu ni kujitakia balaa la bure?
Mbona Serikali inapotokea mgogoro wa wakristo (kumbuka Arumeru) haraka inakwenda kusuluhisha? Wale wanaojidanganya kwamba masuala ya waislamu waachiwe wenyewe hawaoni kwamba madhara wanapata wote? Wasio na walio waislamu?
Jikoni hakuwezi kuwa panawaka moto na walio sebuleni wakaendelea kutazama TV wakidhani masuala ya jikoni hayawahusu! Angalia sasa, wanaolalamika au kuathirika zaidi ya wote ni waislamu au wakristo?
Tunaishi nyumba moja, kama mmoja wa wanafamilia ana malalamiko wanafamilia wanapaswa kukaa pamoja kusikiliza, kushauri na ikibidi kuondosha visababishi vya malalamiko.
Baba wa familia anapaswa kuongoza kikao hicho cha familia na si kuwaachia kila mtoto kumjibu mwenzio anavyoona inafaa! Na hii isiwe tu kwa waislamu bali kwa dini zote ikiwepo na ya kikristo, wahindu, nk.
Tukiendelea kutegemea eti Serikali iwalete FBI au CIA na wengineo kama ndio suluhisho, tutaangamia! Ukishaona nyumba inashindwa kutatua matatizo ya wanafamilia hadi wamwite jirani wa mbali, ujue hiyo familia haiko salama!
Uongozi dhaifu
Uongozi ambao hautambui kuwa kauli na vitendo vyake vinaweza kuchochoea ubaguzi ni uongozi dhaifu sana. Sasa viongozi wetu wamefanya nyumba za ibada (hasa makanisa) ni maeneo yao ya kazi au kuendesha kampeni.
Ukishakuwa kiongozi wewe ni kiongozi wa wote; wa imani na wasiokuwa wa imani yako. Wewe nenda siku na saa yako ya ibada kafanye ibada yako, full stop!
Kisingizio cha kuchangisha harambee hakina mashiko. Ni udini tu! Hivi nani alikuwa Mkatoliki kama Mwalimu Nyerere? Yeye mbona hatukumuona akizunguka toka kanisa moja kwenda jingine kwa kisingizo cha kuchangisha mamilioni yeye na marafiki zake?
Hivi sasa mshiriki mkuu kwenye hizi harambee ni Mkristo; hivi ingekuwaje au itakuwaje akijitokeza muislamu mwenye ndevu akaanza kuzunguka nchi nzima misikitini akichangisha mamilioni? Hatutamwitia CIA au FBI? Hatutamwita majina ya Al Shabaab, Al Qaeda?
Tusiwaonee haya viongozi wa aina hii. Tuwaambie wao na wanaowakaribisha bila kubabwaja kuwa ‘MCHEZO WAO NI MAUTI YETU’!
Uongozi imara pia hauwezi kuruhusu nyumba za ibada zianzishwe kama uyoga hata kwenye mabanda ya kuku!
Tanzania ni nchi pekee unaweza kuanzisha msikiti au kanisa kwenye nyumba yako bila kusajiliwa na serikali eti tunajidanganya serikali haina dini!
Serikali yetu haina dini lakini ina wajibu wa kuhakikisha wenye dini wanafuata sheria na wanaishi kwa amani na upendo!
Serikali yenye kujua itendalo haiwezi kuachia shughuli za imani moja ikaendeshwa ndani ya maeneo ya umma kama mabasi, kumbi za mikutano nk.
Inakera, wewe umelipa nauli halafu unaingia ndani ya basi mtu anaanza kwaya au kaswida? Na tuambizane ukweli, wa kwaya ndio wamekubuhu! Au unaweka mkanda wenye maudhui ya dini fulani ukiuliza unaambiwa kama hufurahishwi usitizame?
Serikali imara inapaswa kupiga marufuku tabia hizi na hata za kuandika maandishi ya kiimani ubavuni mwa vyombo vya usafiri.
Wakati wa Mwalimu Nyerere  hata hakupata taabu mzee wa watu; maana wenye vyombo vya usafiri hawakuthubutu kwa kuwa walielimishwa ubaya wa udini!
Hivi inasaidia nini kuandika ‘gari hili linalindwa na damu ya Yesu’? Au ‘Mwenye ezi Mungu ni Mmoja na Muhamad (SAW) ni mtume wake’? Haitoshi kauli hizi kukaa moyoni mwako na ndani ya nyumba yako au nyumba ya ibada yako?
Kama nilivyosema awali, haya mambo hayakuwapo enzi zile za Mwalimu Nyerere lakini kwa kadri tulivyoyaruhusu sasa yamepamba moto. Magazeti na vituo vya TV vimeanzishwa na kazi ni moja na wote tunaijua ila tunajifanya hamnazo!
Serikali yenye kujua uzito wa kulea udini haiwezi kuruhusu mtu aote ndoto kwa imani ya dini fulani na Serikali imsaidie kutibu wananchi kutokana na ndoto!
Aidha, viongozi wa Serikali inayojua wajibu wake hawawezi kuwa mstari wa mbele kuwaaminisha wananchi kuwa dawa hiyo ya kiimani inatibu bila kufanyiwa utafiti na vyombo ilivyounda yenyewe!
Uongozi imara hauwezi kuruhusu maandishi na vitabu vya dini kuingizwa kwenye ofisi zake. Sasa hapo Tanzania hakuna ofisi ya umma utaingia usiweze kubaini mara moja mhusika ni wa dini gani!
Bila aibu wamebandika maadiko ya imani zao kwenye kuta za ofisi za umma! Mathalani weye ni mkristo, unaingia ofisi unakuta nyuma ya kiti alichokalia bosi kumeandikwa ‘ Ashadu Alla illah Hai La Lah, wa ashadu anna Muhamadan Rasullulah’! Imani inakutoka mara moja kama utaweza kupatiwa huduma ofisi ile.
Halikadhalika unaingia ofisi ya umma unakuta maandishi ‘BWANA NDIYE KIMBILIO LANGU’! Unaanza kujiuliza sijui nimwamkie ‘bwana asifiwe’ ndio nitahudumiwa?
Serikali tuondosheeni upuuzi huu katika ofisi za umma. Wengine wamekubuhu kiasi wanaruhusu vikundi vya maombi kutembelea ofisi za umma kutoa maombi!
Utasikia mtumishi anawaomba wenzie: “Jamani watumishi wa mungu wametutembelea, karibuni tufanye maombi. Haitachukua muda mrefu’! Jamani, kama mtu anataka kutumikia imani yake aende kanisani au msikitini akaombe kazi huko!
Mahubiri ya chuki ndani ya nyumba za ibada, majumbani mwetu, ofisi za serikali, taasisi za elimu na kwenye vyombo vya habari.
Ukitaka kujua chuki haianzii kwenye mihadhara bali inaanzia ndani ya nyumba za ibada wewe nenda kwenye nyumba zetu za ibada hata kama hazina spika usikilize watoto wanavyofundishwa ubaya wa dini nyingine!
Sasa ni mashindano ya kueleza ubaya wa imani nyingine na si kutoa mafundisho ya kitabu cha imani husika.
Wajuzi wanasema ‘a child is the reflection of the parents’. Ukitaka kujua watoto wanaelimishwa nini majumbani jaribu kumuuliza mtoto ni nini mtazamo wake kwa watu wa imani nyingine! Utasikia chuki na dharau.
Watoto wa aina hii ndio hao wanaokojolea vitabu vitakatifu bila woga! Mie miaka ile japo nimetoka familia ya kiislamu sikuwaza hata siku moja kumtukana mkristo au kukashifu Biblia!
Nilisoma shule ya msingi ya Waluteri (Makuyuni Lutheran Primary School), na hakuna mchungaji au mwanafunzi wa kikristo alinikashifu au kunitaka niache usilamu niwe Mluteri kwa miaka yote saba niliyosoma pale!
Sikuwahi pia kusikia mtoto wa kikristo akimtukana mwislamu au akikashifu uislamu. Sote tulihubiriwa vyema kwenye nyumba za ibada na tulilelewa vyema na wazazi wetu.
Ilifika mahali tulivutiwa hadi kila asubuhi wenzetu walipokuwa wanaenda kanisani kwa sala ya asubuhi tuliongozana nao kuwalinda wasidhuriwe na wanyama!
Ndugu zangu, huu utamaduni wa kupandikiza chuki ndani ya mioyo ya watoto na vijana utatugharimu! Si kumtumikia mungu huku; bali ni kumtumikia shetani!
Ndugu zangu, hata tukifuta mihadhara haitasaidia sana. Bila kutibu haya itakuwa sawa na nyumba inayovuja halafu mwenye nyumba anaamua kuhamisha kitanda toka kona hii kwenda kona ile.
Ili tupone ugonjwa huu unaotutafuna, lazima tutibu vyanzo na si dalili. Mihadhara, kuchinjana, kutukanana, kukashfiana, kuchoma na kunajisi vitabu vitakatifu, kupigana risasi na kumwagiana tindikali ni dalili (symptoms) tu!
Ukiondoa dalili bila kuondosha vidudu viambukizi (infectious agents) ugonjwa hauponi ng’o! Tutapiga marufuku mihadhara na tutaona chuki na matendo ya chuki yakishamiri.
Taifa linatakiwa lisimame na kutoa ufumbuzi kwa niliyoeleza hapo juu. Lazima tupige marufuku siasa za maji taka, tushughulikie malalamiko ya waumini kwa dhati, tusiruhusu dini moja kuchukua jukumu la serikali kujibu malalamiko ya dini nyingine.
Aidha,  tuzuie matendo, maandishi, nyimbo, sinema na mahubiri sehemu za umma, uanzishwe utaratibu wa kuanzisha nyumba za ibada na tuwahimize waalimu wa shule za madhehebu, wamiliki wa vyombo vya habari, wazazi na viongozi wa dini kuacha mahubiri au malezi yanayopandikiza chuki miongoni mwa watoto na vijana.
Aidha, uwekwe utaratibu wa kufuatilia na pale inapobainika kuna ukiukwaji mhusika aadhibiwe mara moja.
Lakini jukumu hili lisiachiwe Serikali peke yake. Viongozi wa dini, wazazi na kila moja wetu ajiulize hivi kupalilia chuki dhidi ya dini au madhehebu nyingine inatusaidia nini? Je, hatuvuni hasara badala ya faida?
Kwa nini tusihubiri yale yaliyo mema kwenye imani zetu na kusisitiza umuhimu wa kuvumiliana?
Tunapaswa kujua hakuna aliye bora mbele ya mwenye ezi Mungu zaidi ya yule aliye mwema miongoni mwetu. Na kamwe haitatokea watu wote tukawa wa utakuwa unaota ndoto za alinancha.
"CHANZO GAZETI LA RAIA MWEMA"

 

0 comments:

Post a Comment