Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 2 May 2013

TUHUMA:Vigogo, wakalia mabilioni ya CIS

Baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara na wizara kadhaa za Serikali za Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wameendelea kukalia mabilioni ya shilingi waliyokopa kupitia uliokuwa Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka nje ya Nchi (Commodity Import Support - CIS).
Taarifa ambazo zimelifikia Mwananchi zinasema kiasi cha fedha ambacho bado hakijarejeshwa na wakopaji hao ni Sh216 bilioni ambazo kama zingepatikana, zingetosha kugharimia madawati milioni 2.7 kwa gharama ya Sh80,000 kila moja yenye uwezo wa kutosheleza wanafunzi milioni 8.1.
CIS ni mpango ulioanzishwa na Serikali miaka ya 1980 na kuendelea hadi mwanzoni mwa miaka 2000, ambao nchi wahisani zikiongozwa na Japan zilikuwa zikiipatia Serikali fedha za kigeni ili kuimarisha sekta za biashara.
Nchi nyingine zilizochangia fedha hizo ni Uingereza, Uholanzi, Saudi Arabia, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Sweden na Denmark na madeni yaliyotokana na fedha hizo ni sehemu ya deni la taifa ambalo linagharimiwa na fedha za walipakodi wa sasa.
Hata hivyo, taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mpango huo ni kama ulihujumiwa na baadhi ya waliochota fedha hizo kwani walizitumia kinyume cha makusudio na sasa ni kama Serikali imeshindwa kuzirejesha licha ya kumwajiri mkusanyaji kwa mwaka mzima.
Fedha hizo zilitakiwa kutumika kununulia malighafi, vyombo vya usafiri wa barabara, vifaa vya kilimo na ujenzi, wakati huo hali ya uchumi hususan ya upatikanaji wa fedha za kigeni ilikuwa mbaya, hivyo mpango huu ulikuwa usaidie kuinusuru hali hiyo.
Mwanzoni mwa 2011, Serikali iliingia mkataba wa mwaka mmoja na kampuni ya udalali ya Msolopa Investiment Limited ambayo kwa mujibu wa taarifa za uhakika, mkataba wake ulimalizika Januari mwaka jana bila kutimiza lengo la kurejesha mabilioni hayo.
Mkataba huo ulifikia ukomo huku Msolopa ikiwa imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh5 bilioni, sawa na asilimia 2.31 tu ya Sh216 bilioni ambazo bado zinadaiwa mikononi mwa wakopaji.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msolopa, Ibrahim Msolopa alikataa kuzungumzia suala hilo akisema hana mamlaka...
“Mkataba wangu na Serikali juu ya suala hilo ulishafikia ukomo, nimeshakabidhi kila kitu kinachohusu CIS kwa Serikali kwa hiyo kama mnahitaji taarifa yoyote nendeni serikalini.”
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema halifahamu suala la watu kudaiwa fedha za CIS... “Ninahitaji muda wa kulifuatilia suala hili na kufahamu undani wake.”
Vigogo wanaodaiwa
Uchunguzi umebaini kuwa fedha hizo zimekaliwa na wafanyabiashara na wanasiasa kupitia kampuni zao wakiwamo wabunge wa CCM, Abbas Mtemvu (Temeke) na Henry Shekifu (Lushoto), Wenyeviti wa CCM wa mikoa, Ramadhan Madabida (Dar es Salaam) na Adam Kimbisa (Dodoma).
Kampuni ya Shamshi & Sons ya Shekifu ilikopa Yen za Kijapani 12,778,082.81 (sawa na Sh.207 milioni) kwa kuzingatia viwango vya sasa vya kubadilisha fedha ambavyo ni wastani wa Sh16.20 dhidi ya Yen moja.
Kampuni ya Cargo Plan International, ambayo mmiliki wake ni Kimbisa ilikopa Yen 2,882,961.79 (zaidi ya Sh46.7 milioni), wakati Tanzania Pharmaceutical inayomilikiwa na Madabida ilikopa Yen 7,031,983.29 (takriban Sh114 milioni).

0 comments:

Post a Comment