Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 28 May 2013

Rage ashauri kuminywa uhuru wa habari nchini




 Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Aden Rage, ameitaka serikali kuongeza ada ya usajili wa magezeti hadi kufikia Sh. milioni 500 badala ya Sh. 500,000 ilivyo sasa.

Rage alitoa kauli hiyo jana Bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza, akiitaka serikali kuongeza ada ya usajili hadi kufikia Sh. milioni 500 kama ilivyo kwa nchi za jirani badala ya 500,000 kwa gazeti moja kusajiliwa.

“Pia, waziri atakubaliana nami kuwa magazeti mengi yamekuwa yakiandika habari nyingi za uchochezi na huu ni wakati muafaka wa kuchukua hatua kali kwa wale wote wanaoleta vurugu nchini” alisema.

Akijibu, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alisema Tanzania ina magazeti mengi ambayo yanaandika habari mbalimbali.

Alisema suala hilo la kuongeza ada wanaliangalia ili kuhakikisha kwamba ada inaongezeka wakati wa Sheria ya Vyombo vya Habari itakapowasilishwa Bungeni.

“Basi suala hili linatakapokuja Bungeni wabunge wenzetu tunaomba mtusaidie kulipitisha na kuweka misimamo ambayo inaeleweka, ili wale wamiliki wa magazeti waweze kuchukua umuhimu kuwa wanawajibika kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Kuhusu magazeti kuandika uchochezi, alisema, serikali inaliona jambo hilo na kudai kwamba wananchi na wabunge wamekuwa wakilalakia suala hilo.

Alisema serikali inawashauri wale wote ambao wamepata matatizo hayo kuchukua hatua za kisheria dhidi ya magazeri husika, wahariri, waandishi na wachapishaji.

Waziri alisema anayetaka kusajili magazeti huwasilisha barua ya maombi kwa Msajili wa Magazeti huku akieleza jina pamoja na madhumuni ya gazeti husika.

Alisema mwombaji baada ya kutimiza masharti hayo, anatakiwa kulipa ada ya usajili Sh. 500,000 na kisha hupewa hati ya usajili.

Aidha, alisema Tanzania ina jumla ya magazeti 780 ambayo yamesajiliwa kwa mujibu wa sheria.

0 comments:

Post a Comment