Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 21 May 2013

Msigwa, wenzake 49 wapata dhamana
 Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa jana alipandishwa kizimbani pamoja na watu wengine 76 na kusomewa mashtaka matatu kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Wilaya ya Iringa.

Mchungaji Msigwa anashtakiwa kuhusika katika vurugu zilizotokea juzi mjini Iringa kuhusu mgogoro baina ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na wafanyabiashara kwenye eneo la Mashine Tatu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Msigwa aliachiwa kwa dhamana ya Sh1 milioni na wenzake 49 huku wengine 27 wakirudishwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Godfrey Isaya, Mwendesha Mashtaka, Adolph Maganda alisema Mchungaji Msigwa aliwashawishi watu kufanya kosa kwenye eneo la Mashine Tatu kinyume cha sheria, kushiriki katika mkusanyiko ambao haukuwa na kibali.
Hata hivyo, Msigwa ambaye anatetewa na Wakili wa Kujitegemea, Basil Mkwata hakuhusishwa na shtaka jingine la kuharibu mali kwa kukusudia, ambalo linawahusu wenzake kuanzia wa pili hadi wa 76.
Pia watuhumiwa hao wa pili hadi wa 76, walihusishwa katika shtaka la pili la kushiriki kwenye mkusanyiko lakini hawakujumuishwa kwenye shtaka la kwanza.Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 3, mwaka huu.
Ulinzi mkali
Mchungaji Msigwa na wenzake walifikishwa mahakamani saa saba mchana wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Mbali ya mahakamani, ulinzi pia uliimarishwa katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Iringa ambako Mchungaji Msigwa na wenzake walikuwa wamewekwa.
Wafuasi wa mbunge huyo walifurika kwenye kituo hicho na baadaye kwenda mahakamani hali iliyowafanya polisi kuongeza ulinzi wa magari yenye maji ya kuwasha.
Baada ya kuachiwa kwa dhamana saa kumi na moja jioni, Mchungaji Msigwa alibebwa juujuu na wafuasi hao ambao walimsindikiza kwa maandamano yaliyopita barabara mbalimbali za Iringa hadi Ofisi za Chadema Mkoa wa Iringa eneo la Mshindo.
Mbunge huyo aliwashukuru wafuasi wake na kuwaahidi kuwa ataendelea kutetea haki zao licha ya kufunguliwa mashtaka... “Nitawasaidia wale wote waliobaki rumande ili kukamilisha masharti ya dhamana.”

0 comments:

Post a Comment