Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 21 May 2013

JK: Lowasa jembe



 Rais Jakaya Kikwete amemwagia sifa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hatua ambayo inaweza kutafsiri mengi katika medani ya siasa nchini.

Akizungumza na wabunge wa CCM kwenye Ukumbi wa White House Dodoma juzi, Rais Kikwete ambaye pia mwenyekiti wa chama hicho, alisema nguvu za Lowassa pekee zinatosha kushinda uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani Kata ya Makuyuni kilichoko wilayani Monduli.
Kata ya Makuyuni iko wilayani Monduli, ambako Lowassa amekuwa mbunge wake tangu mwaka 1995.
Habari za kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Rais Kikwete alitoa kauli hiyo kuhusu kampeni za uchaguzi huo wa Makuyuni, baada ya kuwa ametoa ruksa kwa makada wa chama hicho wanaotaka urais kuanza kujipitisha pitisha miongoni mwa wanachama wa chama hicho. Lowassa anatajwa kuwa miongoni mwa wanaCCM wanaotaka kumrithi Rais Kikwete kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
“Sina tatizo na pale Makuyuni, najua muscles (misuli) za Mzee Lowassa zinatosha kutupa ushindi; au vipi mzee?” alidokeza mmoja wa wabunge wa CCM akimnukuu Rais Kikwete.
Uchaguzi wa Udiwani Kata ya Makuyuni unaotarajiwa kufanyika Juni 16, mwaka huu, utakuwa wa ushindani mkali kati ya CCM na Chadema ambao historia yao kisiasa mkoani Arusha ni ya uhasama.
Katika uchaguzi huo, unaofanyika baada ya kifo cha Abdillah Warsama (CCM), chama hicho kitatetea nafasi yake kwa kumsimamisha Godluck Lerunya na Chadema ni Japhet Sironga.
Mbali na Kata ya Makuyuni, uchaguzi wa udiwani mkoani Arusha utafanyika pia katika Kata za Kaloleni, Themi, Kimandolu na Elerai, kutokana na waliokuwa madiwani wa kata hizo (Chadema), kufukuzwa na chama chao.
“Mnaweza kuchafuana leo, kesho mkapata mgombea mwenye nundu nyingi na mabandeji kila mahala, halafu mkapata shida kumnadi,” alisema.
Siyo mara ya kwanza kwa Kikwete kumsifia Lowassa kwani aliwahi kufanya hivyo mwaka jana huko Longido wakati akikabidhi ng’ombe.
Pia aliwahi kumsifia wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2010 wakati Kikwete alipomwelezea Lowassa kama Mbunge makini na kuwaomba watu wa Monduli kumchagua tena.
Hata hivyo, alipoulizwa kama baada ya kuruhusiwa kuanza kujipitisha kwa wanaCCM kama anataka kuwania urais, Lowassa alijibu kupitia watu wake wa karibuni kuwa asingependa kuzungumzia suala hilo hasa baada ya Rais kutoa kauli hiyo.

0 comments:

Post a Comment