Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 2 May 2013

JK atangaza neema kwa wafanyakazi


Rais Jakaya Kikwete ametangaza neema kwa wafanyakazi baada ya kuahidi kuwa Serikali itawapunguzia makato ya kodi (Paye) na pia itawaongezea mishahara.
Akihutubia taifa katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mjini Mbeya jana, Rais Kikwete alisema Serikali imeitikia   kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi.
Aliahidi kuwa Serikali itatangaza punguzo hilo la ongezeko la kodi na mishahara kwa watumishi wa umma wakati Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa atakapowasilisha Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa  Fedha wa 2013/14.
Pia alisema Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka atatangaza nyongeza ya mshahara kwa sekta binafsi atakapowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Serikali kupunguza kodi hiyo kwani mwaka 2007, iliipunguza kutoka asilimia 18 hadi 15  na mwaka 2010 iliipunguza tena hadi asilimia 14.
Rais Kikwete alisema mfumo wa makato ya kodi unatokana na kipato cha mtu jambo ambalo limechangia wengine kukatwa kiasi kikubwa na wengine kidogo lakini akasema anaamini kuwa makato hayo yataendelea kupungua bila ya kuathiri uchumi wa nchi.
Mishahara
Rais Kikwete alisema kuwa katika bajeti hiyo, Serikali itatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma na sekta binafsi huku akiahidi kuwa italingana na hali halisi ya maisha.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali imetenga zaidi ya Sh4.76 trilioni katika Bajeti ya Mwaka 2013/14 kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi wa umma.
Alisema katika Bajeti hiyo, asilimia 44.9 ya fedha itakuwa kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi, fedha ambazo zitatoka katika vyanzo vya mapato vya ndani.
Alisema katika kiasi hicho, zaidi ya asilimia 4.9 zinatoka kwenye mapato ya Serikali na kilichobaki kitatoka kwenye vyanzo mbalimbali.
“Tunajua kuwa, mishahara ya wafanyakazi ni midogo, lakini Serikali imekuwa ikijitahidi kuongeza kila mwaka ili iweze kuendana na hali halisi ya maisha,” alisema.
Alisema mwaka juzi, kima cha chini kilikuwa Sh65,000 ambacho kiliongezwa hadi kufikia Sh125,000 na kwamba mwaka huu wataongeza kiasi kikubwa ili kiweze kukidhi mahitaji.
Mifuko ya Jamii
Akizungumzia kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Rais Kikwete aliwaondoa hofu wananchi na kusema iko hai na wafanyakazi watakaostaafu watalipwa mafao yao kama kawaida.
Alisema utafiti uliofanywa hivi karibuni na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), umebaini kuwa mifuko hiyo haina matatizo yoyote.
Alisema Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), ulikuwa na matatizo ambayo yalianza kabla ya mwaka 1999, jambo ambalo lilifanya uwe na madeni ya zaidi ya Sh6 trilioni. Baada ya kuona hivyo, alisema Serikali iliweka utaratibu wa kuuchangia kiasi cha Sh50 bilioni kila mwaka katika mapato yake.
Alisema kutokana na hali hiyo fedha hizo ndizo zinazotumika kulipa wafanyakazi na wastaafu mafao yao na kwamba mpaka sasa   hakuna aliyelalamika kutolipwa mafao yake.
“Naomba niwaondoe hofu Watanzania wenzangu. Hakuna mfanyakazi atakayekosa kulipwa mafao yake pindi anapostaafu katika mifuko ya hifadhi ya jamii ukiwemo PSPF,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa uwekezaji katika mifuko hiyo unakua siku hadi siku.
Rais Kikwete aliwashauri waajiri kuwaacha wafanyakazi wajiunge na mfuko wowote wanaotaka ili waweze kuhifadhi mafao yao.

0 comments:

Post a Comment