Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 2 May 2013

Dk Shein atangaza Tume mpya ya Uchaguzi Z'bar

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, ametangaza Tume mpya ya Uchaguzi itakayoratibu na kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, uteuzi huo unaanzia Aprili 30, mwaka huu.

Taarifa ilisema Kamishna mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jecha Salim Jecha, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo.

Aidha, wajumbe pekee walioteuliwa kwa mara nyingine katika tume hiyo ni Nassor Khamis Mohamed na Ayoub Bakari Hamad, kutoka Chama cha  Wananchi (CUF).

Wajumbe wapya walioteuliwa katika tume hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, Katibu Mkuu mstaafu wa iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Salmin Senga Salmin, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Haji Ramadhan Haji na Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Abdulhakim Ameir Issa.

Mwenyekiti pamoja na wasaidizi wake, wanatarajiwa kuapishwa Mei 4, mwaka huu na tume hiyo ya uchaguzi inakabiliwa na zoezi la kusajili wapiga kura wa kudumu waliofikisha umri wa miaka 18 baada ya zoezi hilo kukwama kufanyika tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Aidha, tume hiyo itakuwa na kazi kubwa ya kuratibu na kusimamia uchaguzi mkuu wa kwanza ukiwa chini ya mfumo mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoundwa na vyama vya CCM na CUF.

Wakati huo huo, Dk. Shein amefanya mabadiliko madogo kwa kumuondoa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Mustapha Ibrahim na kumteua Dk. Idrisa Muslim Hija kuwa Mkuu wa Mkoa huo wa Kusini Unguja.
 

0 comments:

Post a Comment