Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 23 May 2013

Askari waliombambikizia raia kesi wafukuzwa kazi

Siku chache kufuatia askari wa tatu wa Jeshi la Polisi wa kituo cha Dumila wilayani Kilosa na Dakawa wilayani Mvomer, mkoani Morogoro kutuhumiwa kumbambikizia kesi mfanyabiashara Samson Mwita maarufu kama Mura, mkazi wa Dumila kuwa alikutwa na fuvu la kichwa cha binadamu,  hatimaye askari hao wamefukuzwa kazi rasmi na kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Jeshi hilo limesema askari hao wamefukuzwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fausitine Shilogile,  ilisema hatua hiyo imefikiwa baada ya uchuguzi kukamilika na askari hao kubainika kufanya upekuzi kwa mfanyabiashara huyo bila kuwa na kibali kutoka kwa wakuu wao wa kazi.

Alisema askari hao walifikishwa katika mahakama ya kijeshi na kubainika kufanya kitendo hicho na kuvuliwa uaskari na kwamba tayari wamefikishwa katika mahakama ya kiraia na kesi yao kwa mara ya kwanza inatarajiwa kusomwa Juni 3 katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro.

Aliwataja askari hao kuwa ni mwenye namba D 4807  D/SSGT Sadick wa kituo kidogo  cha Polisi Dakawa, E 4344  SGT Mohamed  na E 3821 CPL Nuran wote wa kituo kidogo cha polisi Dumila.

Alisema kuwa askari hao walifanya tukio hilo  Mei 7, mwaka huu majira ya asubuhi katika kijiji cha Mgudeni Dumila wilayani Kilosa kwa kujaribu kumbambikizia kesi ya kukutwa na fuvu la kichwa kinachodaiwa kuwa cha binadamu mfanyabiashara huyo kwa lengo la kujipatia fedha.

Alisema uchunguzi  umebaini kuwa askari hao walifanya kitendo hicho kwa kushirikiana na raia  Rashidi Ally (47)mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment