Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 18 April 2013

Wekeni wazi gharama za matibabu kuondoa malalamiko'

 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imeitaka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kubandika kwenye mbao za matangazo gharama za matibabu, ili kuondoa utata wa baadhi ya gharama zinazozua malalamiko.

Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donald Mmbando, alitoa agizo hilo jana, wakati akifungua maonyesho ya siku tatu ya huduma za hospitali hiyo katika kuadhimisha miaka 13 tangu iwe Hospitali ya Taifa.

Alisema ni vizuri gharama hizo zikawekwa wazi kuliko kuwaeleza wagonjwa kwa mdomo, kunakozua malalamiko ya baadhi ya watumishi kubambikia bei wagonjwa.

“Muwe wawazi kwenye huduma zenu, unakuta kipimo ni Sh. 100,000 lakini mgonjwa anatozwa Sh. 200,000, kuondoa hili gharama zote za matibabu zibandikwe kwenye mbao za matangazo, iwe rahisi kwa wagonja au ndugu zao kuzisoma,” alisema.

Aidha, alisema serikali inashirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha huduma za afya nchini hususan kwenye hospitali hiyo, ili kupunguza idadi ya Watanzania wanaogharimiwa kwenda nje ya nchi.

“Hospitali hii ni tegemeo kubwa sana kwa Watanzania wengi, asilimia 60 watibiwa kwenye hospitali za serikali na asilimia 40 binafsi na za taasisi za dini,” alisema Dk. Mmbando.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk. Marina Njelekela, alisema mapato ya ndani yameongezeka kwa asilimia 18, tangu uanzishwe utaratibu wa malipo kupitia benki ya NMB.

Alisema Muhimbili inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uwezo wa kifedha mdogo ukilinganisha na majukumu inayotakiwa kutekeleza.

Mkurugenzi huyo alisema nyingine ni sera ya msamaha ambayo imeongeza wagonjwa, tatizo la upatikanaji wa baadhi ya madawa katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kutokana na hadhi ya ubingwa wa juu.

Nyingine ni upungufu wa wafanyakazi hasa kada ya wauguzi na wataalumu katika maeneo muhimu ya kibingwa kama tiba ya moyo, nusu kaputi na upasuaji wa watoto.

0 comments:

Post a Comment