Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani limetoa wito wa kushtakiwa
wafuasi wapya wa fikra za unazi nchini humo kwa tuhuma za kuwaua
wahajiri kadhaa wa kigeni katika nchi hiyo. Duru za habari zinaripoti
kutoka Munich Ujerumani kwamba, Aiman Mazyak Mwenyekiti wa Baraza Kuu la
Waislamu nchini Ujerumani ametoa wito kupandishwa kizimbani wafuasi
wapya wa fikra za unazi nchini humo ambao wanatuhumiwa kuwaua wahajiri 9
wa Uturuki na Ugiriki. Aiman Mazyak amesema, Waislamu wa Ujerumani wana
matumaini kwamba, kwa kuwa sheria ni msumeno basi itafanya kazi yake na
wafuasi hao wa unazi kupandishwa kizimbani kujibu kesi ya mauaji.
Mahakama ya Katiba ya Ujerumani jana ilitoa amri ya kuandaliwa mazingira
kwa ajili ya kuweko katika ukumbi wa mahakama waandishi wa habari wa
Kituruki na Kigiriki. Aiman Mazyak Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu
nchini Ujerumani amesema kuwa, kuandaliwa mazingira ya kuhudhuria kesi
hiyo waandishi hao wa habari isiwe sababu ya kuakhirishwa kesi hiyo.
Ikumbukwe kuwa, genge la watenda jinai nchini Ujerumani linalojulikana
kwa jina la Zwickau ambalo linafuata fikra za Kinazi liliwaua wahajiri 8
wa Kituruki na Mgiriki mmoja baina ya mwaka 2000 na 2007 kwa chuki za
kibaguzi.
Sikiliza Live
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment