Mkakati wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wa ujenzi wa nyumba 15,000; zikiwamo 5,000 za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali nchini, umepamba moto, baada ya NHC na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), kutiliana saini makubaliano ya utoaji wa mafunzo kwa vijana 35 ya kutengeneza matofali kwa ajili ya mradi huo.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema jana kuwa vijana
hao; wakiwamo wanaume 32 na wanawake watatu, ni kati ya 60 waliotafutwa
na Veta kutoka mikoa 16 ya Tanzania Bara, ambayo kwa sasa ina ujenzi wa
nyumba za gharama nafuu.
Mchechu alisema hayo katika hafla ya utiaji saini makubaliano na
uzinduzi wa mafunzo hayo kwa vijana hao, iliyofanyika Veta, jijini Dar
es Salaam jana.
Alisema Veta kwa kushirikiana na NHC, iliwachuja vijana 60 kupitia
usaili makini uliofanyika wiki iliyopita na kuwabakisha 35, ambao
watatafundishwa kwa wiki mbili kuanzia jana, kutengeneza tofali kwa
kutumia teknolojia mpya ya mashine za “Hydraform”.
Mchechu alisema anatarajia ushirikiano uliowezesha kuwapata vijana
hao, utakuwa na manufaa makubwa kwa kuwa utawezesha ujenzi wa nyumba
1,054 ndani ya mwaka mmoja na kwamba matofali 5,270,000 yenye gharama ya
Sh. bilioni 3.162 yatatengenezwa na vijana hao.
Aliwahakikishia vijana hao kuwa baada ya kumaliza mafunzo yao
watawachukua kwa mkataba wa mwaka mmoja na kuwapeleka katika maeneo
ambayo watashiriki kufyatua matofali na kujenga nyumba za gharama nafuu.
Awali, Mkurugenzi wa Uendelezaji Milki wa NHC, Benedict Kilimba,
alisema baada ya kupata mafunzo hayo, vijana hao watasambazwa katika
mikoa mbalimbali, ikiwamo Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tanga,
Singida, Manyara, Lindi, Kigoma, Ruvuma na Katavi, kufanya kazi hiyo.
Mchechu alisema mashine 15 za aina hiyo zimenunuliwa na kwamba kila moja ina uwezo wa kufyatua tofali 2,000 kwa siku.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Zebadiah Moshi, alisema tatizo la
ajira kwa vijana limekuwa kilio kikubwa nchini, hivyo hatua hiyo
itasaidia kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, alisema kulingana na utafiti uliofanyika kwa miaka
mitatu, kati ya vijana wanaomaliza vyuo, asilimia 66 hupata ajira na
kwamba, wanapenda iongezeke kufikia asilimia 95 katika kipindi cha miaka
mitano.
0 comments:
Post a Comment