Uhuru Kenyatta ameapishwa leo kuwa Rais wa Nne wa Kenya katika sherehe
iliyohudhuriwa na makumi ya maelfu ya wafuasi wake waliojawa na furaha
pamoja na viongozi zaidi ya 20 kutoka nchi kadhaa za Afrika. Katika
hotuba yake baada ya kula kiapo, Kenyatta ambaye ni mwana wa Rais wa
Kwanza wa Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta amesema atawahudumia Wakenya
wote pasina kuwepo ubaguzi. Ametoa wito kwa Wakenya wote kudumisha umoja
na amani. Rais Kenyatta amesema katika siku 100 za kwanza za utawala
wake ataondoa malipo ya huduma za uzazi na halikadhalika wananchi
watapata matibabu katika zahanati za serikali pasina kutoa malipo. Vile
vile amesema shilingi bilioni sita ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili
ya duru ya pili ya uchaguzi zitatumika kuanzisha mfuko mpya wa vijana na
wanawake kote nchini Kenya. Amesema, serikali yake itabuni nafasi za
kazi hasa kwa ajili ya vijana. Kuhusua masuala ya kimataifa amesema
Kenya itaheshimu majukumu yake ya kimataifa kwa msingi wa kuheshimiana.
Amesema hakuna nchi yoyote inayopaswa kuhodhi au kudhibiti taasisi za
kimataifa au kufasiri mikataba ya kimataifa. Amesema kila nchi ina haki
ya kuwa na mtazamo wake ambao unapaswa kuheshimiwa na mataifa mengine.
Sikiliza Live
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment