Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 23 April 2013

Uchaguzi mdogo Chambani Juni 16


Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Chambani, Pemba, unatarajia kufanyika Juni 16, mwaka huu.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Salum Hemed Hamis, kufariki dunia  Machi 28, mwaka huu.
 
Aidha, uchaguzi huo utaenda sambamba na wa madiwani katika Kata 26 za Halmashauri 21, kwa ajili ya  kujaza nafasi zilizoachwa  wazi kufuatia baadhi ya waliokuwa wanashikilia nafasi hizo kujiuzulu, kufukuzwa, kuhama vyama au kufariki.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jullius  Mallaba, uteuzi wa wagombea wa kiti cha ubunge utafanyika Mei 17, mwaka huu, kwa kufuatiwa na kampeni  ambazo zitafanyika Mei 18 hadi Juni 15, mwaka huu.
 
Alisema uteuzi wa uchaguzi mdogo wa madiwani utafanyika  Mei 14, mwaka huu, wakati kampeni zitakuwa ni Mei 15 hadi Juni 15, mwaka huu.
 
Kata zitakazohusika katika uchaguzi mdogo wa Madiwani  ni Stesheni (Nachingwea), Nyampu-Lukano na Lugata (Sengerema), Genge na Tingeni (Muheza), Ibugule (Bahi), Langiro (Mbinga), Manchila (Serengeti), Iyela (Mbeya), Mbalamaziwa (Mufindi), Runzewe Mshariki (Bukombe) na Mianzini (Temeke). 
 
Nyingine ni Dalai (Kondoa), Minepa (Ulanga), Makuyuni(Monduli), Bashnet (Babati), Kimandolu, Elerai, Kaloleni na Themi (Arusha), Iseke (Singida), Dongobesh (Mbulu), Ng`ang`ange (Kilolo), Ifakara (Kilombero), Msanze (Kilosa)  na Mnima (Mtwara).
 
Salim Hemed Hamis alifariki dunia katika hospitali ya Taifa Muhimbili alipolazwa siku moja baada ya kuanguka ghafla wakati akishiriki katika vikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 

0 comments:

Post a Comment