Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 16 April 2013

TCRA: Hatuwezi kuwadhibiti wanaotumia simu vibaya

06Jumaadal Aakhir,1434 Hijiriyah/ April 16,2013 Miyladiyah


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema Jeshi la Polisi nchini ndilo lenye mamlaka ya kuwakamata watu wanaohusika kutuma ujumbe mfupi wa maneno (sms),  kwenye simu zenye uchochezi au utapeli zinazotumwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya simu za mkononi.

Aidha, TCRA imesema haihusiki kudhibiti meseji hizo na kwamba anayeweza kushughulikia jambo hilo ni polisi.

Hayo yalisemwa na Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA,Victor Nkya, alipozungumza na NIPASHE kuhusiana na utapeli unaoendelea kufanywa na baadhi ya watu kupitia simu za mkononi.

Alisema watu wanaotumia simu za mkononi kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ni sawa na mtu analiyefanya kosa la jinai ambaye anapaswa kushughulikiwa na polisi.
Alifafanua kuwa matapeli hao wanatumia simu kama nyenzo ya utapeli na ni sawa na mtu yoyote anayetua kitu kumdhuru mwingine, hivyo anakuwa amefanya kosa la jinai na anapaswa kushughulikiwa na polisi.

Alisema kwa mtu yeyote aliyewahi kutapeliwa fedha au kitu chochote anapaswa kwenda kituo cha polisi akiwa na namba ya simu iliyomtapeli kupata msaada zaidi.

Nkya aliongeza kuwa jeshi la polisi pekee ndilo litakaloweza kumpata mhusika aliyetapeli kwa njia wanazozifahamu hata kama mtu huyo hakuisajili namba yake.

“Jeshi la polisi likishapata namba hiyo, wenyewe ndiyo wanajua namna gani ya kumbaini mhusika huyo,” alisema Nkya.

Aidha, Nkya alisema makosa kama kumtukana mtu, au kumfanyia kitendo chochote ambacho ni kinyume na maadili, mlalamikaji anapaswa kutoa taarifa katika kituo cha polisi kilicho jirani naye kwa msaada zaidi.

Kumekuwapo na vitendo vya utapeli vinavyoendelea katika mitandao ya simu za mkononi vinavyofanywa na baadhi ya watu wakijidai kuwa na shida, huku wakihitaji fedha kwa kutumia majina ya marafiki au ndugu wa wanaowatapeli. Matapeli hutumia pia majina ya viongozi wakubwa serikalini na wabunge.

Hadi sasa watu kadhaa wamekwisha tapeliwa fedha kwa kutumiwa sms na matapeli hao pasipo kufahamu na pindi wanapopigiwa simu hawapokei.

0 comments:

Post a Comment