Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 23 April 2013

TAMKO LA SHURA YA MAIMAMU


 
SHURA YA MAIMAMU (T)

Tamko la Shura ya Maimamu lililotolewa katika Msikiti wa Mtambani tarehe 17/04/2013
SISI viongozi kutoka Shura ya Maimamu inayojumuisha maimamu wa misikiti  iliyosajiliwa hapa nchini, tumelazimika kukutana na kutafakari kwa kina suala la uchinjaji lililoanzishwa na viongozi wachache wa dini ya Kikristo kwa malengo mbalimbali yaliyojificha ikiwemo la kuwaondoa Waislamu kwenye madai yao ya msingi.
Miongoni mwa madai ya msingi kabisa ambayo kwa muda mrefu Waislamu tumekuwa tukiyadai kwa serikali ni pamoja na hoja ya kuweko kwa makubaliano ya serikali kuyapa fedha Makanisa kila mwaka kwa shughuli zao za kimaendeleo chini ya kinachoitwa MoU.
Aidha Waislamu tumekuwa tukidai Baraza la Mitihani lifumuliwe na liundwe upya kwakuwa taswira iliyopo sasa inaonesha kama vile ni kitengo cha Parokia  ya Kikatoliki na kwamba Wasomi Waislamu hawawezi kushika nyadhifa.
Pia suala la Nchi yetu kujiunga na jumuiya za Kimataifa kama vile OIC ni miongoni mwa mambo yanayopigiwa debe sana na Waislamu tokea mwanzoni mwa miaka ya 1990 lakini wahusika wanajibaraguza na kutia pamba masikioni.
Suala la kurejeshewa Mahakama ya Kadhi nalo tumekuwa tukilidai kwa zaidi ya miaka 27 sasa pasi na kupatiwa ufumbuzi kiasi cha kugeuka kuwa  ni kero yetu nyingine ambapo badala ya kutupa, wao wanaipa mamlaka taasisi moja nafasi ya kuteua Kadhi!
Kwa ufupi Waislamu wa Tanzania tuna madai ya nchi kuendeshwa na MFUMO KRISTO ambao unatoa fursa ya nafasi zote za kiutendaji serikalini na taasisi za Umma zishikwe na watu wa DINI moja na kuwafanya Waislamu wajione kama hawana stahiki ya kushika nafasi hizo.
Mfumo KRISTO umepelekea hadi viongozi wa Makanisa wajione wana nafasi pekee ya kusikilizwa na viongozi wa serikali kiasi kwamba kila wanalolitaka ni lazima wahakikishe linatekelezwa.
Mathalani katika hoja hii ya kudai haki ya kuchinja ambayo imeibuliwa na viongozi wachache wa Kikristo tayari imesababisha uvunjaji wa msikiti wa Aqswa huko Tunduma katika wilaya mpya ya Momba mkoani Mbeya.
Kikundi hicho cha wachochezi kilifikia hatua hiyo mara tu baada ya kutolewa kwa tamko la Maaskofu 117 waliokutana jijini Dar es Salaam Machi 19, 2013.
Sehemu ya tamko la Jukwaa la Wakristo katika kipengee namba 2 (b) ilikuwa inasema hivi; tunanukuuu;
“ Kwa mantiki hiyo hapo juu katika kipengele cha a-c, Wakristo wanaitaka Serikali iweke utaratibu wa kugawana machinjio na mabucha kati ya Wakristo na Waislamu ili kila Mtanzania awe huru kujinunulia kitoweo mahali anapotaka. Sambamba na kuitaka Serikali kufanya hivyo, tunawakumbusha Wakristo wote Tanzania kuelewa kuwa watakuwa hawajavunja sheria yoyote ya nchi wakiamua kujichinjia kitoweo chao wenyewe”, mwisho wa kunukuu.
Ndugu zangu, japo Wakristo wanaitaka serikali kuweka utaratibu wa kugawana machinjio na mabucha, sisi Waislamu tunaitaka serikali iweke utaraibu wa kugawana Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kati ya Waislamu na Wkristo, kwakuwa Baraza hilo muonekano wake hauna tofauti na PAROKIA ya Kanisa.
VURUGU ZA WAKRISTO TUNDUMA;
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zilizokusanywa zimethibitisha kuwa vurugu hizo zimesababishwa na utekelezaji wa TAMKO LA MAASKOFU uliofanywa na Wakristo wa wilayani Momba katika mji mdogo wa Tunduma na kupelekea kuvunjwa na kuchomwa moto msikiti wa Aqswa uliopo mtaa wa Mwaka.
Mkuu wa wilaya hiyo Saidaye Abiudi alisema kilichotokea siku ya Ijumaa ya April 29, 2013 ni baadhi ya Wakristo kupeleka maombi kwa Mkurugenzi wa mji wa Tunduma wakitaka suala la kuchinja wanyama lifanywe na wao badala ya Wislamu kama ilivyozoeleka.
Akasema ofisi ya Mkurugenzi wa mji mdogo wa Tunduma iliwajibu kuwa, ombi hilo wamelipokea na watalifanyia kazi kwa kuwasiliana na viongozi wao wa juu kwa maelezo kwamba tatizo hilo hivi sasa limekuwa ni la Kitaifa.
Na hivyo ofisi hiyo ikawalekeza kufuata utaratibu wa zamani wa kuchinja uendelee kama kawaida huku wakisubiri utaratibu mpya.
Kwa mujibu wa DC Abiud ni kwamba, licha ya kupoewa majibu hayo, baadhi ya Wakristo walikwenda kuchinja Ng’ombe wenyewe katika machinjio yaliyopo Tunduma bila ya kusubiri maelekezo mapya ya serikali.
Kuona hivyo ndipo Mkuu huyo wa wilaya ya Momba ambaye pia ni Mkristo alipowaita viongozi Wakristo (Wachungaji) akiwemo Mchungaji Neema Mwamalupa kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la hapo Tunduma kuhudhuria kikao hicho ambacho hakukuwa na muislamu hata mmoja aliyealikwa kiasi cha kutofahamika kilichozungumzwa.
Taarifa zinaendelea kufahamisha kuwa, ilipofika Machi 31, 2013 Jumla ya Ng’ombe 40  walichinjwa katik machinjio ya serikali na kati ya hao 37 walichinjwa  na Wakristo wenyewe,  na Ng’ombe watatu waliosalia walichinjwa na Waislamu!
Afisa mwenye dhamana ya mifugo wilayani humo alifika na kukagua Ng’ombe wale watatu waliochinjwa na Waislamu na baada ya hapo aliondoka.
Kwa hiyo nyama ya Ng’ombe wote hao kwa ujumla wake zilipakiwa pamoja na kusambazwa katika mabucha yanayokadiwa kufikia 25 ya Tunduma, hali iliyopelekea msimamizi wa machinjio hayo ambaye ni Muislamu kutoa taarifa kupitia misiki yote kwamba, Waislamu wasinunue nyama kwa siku hiyo kwa kuwa ni kibudu. Nyama hiyo haikununuliwa kweli na Waislamu  hivyo ikalala mabuchani.
Ilipofika April 1, 2013 Mkuu wa Wilaya ya Momba aliwaita viongozi wa Kiislamu peke yao, akafanyanao kikao.
Taarifa kutoka katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na sheikh wa Wilaya ya Momba Ahmad Omar, Mkuu huyo wa wilaya aliwaambia wajumbe kuwa, wenzao Wakristo wamepeleka kwake mapendekezo ya kutaka kuchinja wanyama wao ili wauze kwenye bucha zao.
Akasema kwakuwa Wakristo hao walionekana kupania hasa katika jambo hilo,  aliwaomba mashekh katika kikao hicho wakubaliane nao kwa hoja kwamba, Wakristo wa Tunduma ni wengi kuliko Waislamu. Lakini pia alitoa hoja kwamba nyama zitakazochinjwa na Wakristo zitauzwa kwenye bucha zao tu!
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya aliwapa mfano mashekh ili kuwashajihisha wakubaliane na hoja yake kuwa, Zanzibar Waislamu wako wengi kuliko Wakristo ndio maana mwezi wa Ramadhani haruhusiwi mtu yeyote kula mchana bila kujali ni Muislamu ama Mkristo!
Kana kwamba haitoshi mwakilishi huyo wa Rais katika eneo hilo la Wilaya mpya ya Momba ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliwaambia Mashekh hao kuwa, hata kwenye katiba ya nchi sula hili la kuchinja Waislamu halipo, hivyo akawataka sana wawakubalie Wakristo!
Pamoja na ushawishi huo wote wa Mkuu wa wilaya, masheikh hawakukubaliananaye na hivyo kikao kikamalizika kwa mtindo huo.
Ilipofika April 2, 2013 Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akaitisha kikao kingine katika ukumbi wa Ukinga Hill Hotel Tunduma, kikao hiki tofauti na vile vikao vya DC Abiud, hiki kilijumuisha viongozi wa pande zote za Waislamu na Wakristo.
Katika kikao hicho pia kulikuwa na viongozi mbalimbali wa wilaya akiwemo Mkuu wa wilaya, kamanda wa polisi wa wilaya (OCD), Afisa Uslama wa wilaya ambao wote ni Wakristo.
Upande wa Waislamu uliwakilishwa na sheikh wa Wilaya ya Momba Ahmad Omar, Katibu wa Bakwata Wilaya Suleiman Bakar, Imam wa msikiti wa Jamaa sheikh Idrisa Kaini, Imam wa msikiti wa Oil Com sheikh Jaffar Ramadhan na Imam wa msikiti wa Muuminuna sheikh Abubakar Zubeir.
Kwa Wakristo waliwakilishwa na Mchungaji wa kanisa la KKKT Neema Mwamalupa, Wachungaji mbalimbali wa makanisa ya Tunduma na Waumini wa Kikristo wapatao 200 hivi wote walipata nafasi ya kushiriki katika kikao hicho cha Mkuu wa Mkoa.
Hoja za Wakristo zilizowasilishwa kwenye kikao hicho na kiongozi wao Mchungaji Mwamalupa zilikuwa hizi;
a) Hawawezi kula nyama iliyochinjwa na Muislamu kwa jina la Allah
b) Ng’ombe wa Wakristo kwanini wasichinje wenyewe?
Kwa upande wa Waislamu walitoa hoja zifuatazo;-
a) Sisi tunachinja kwa jina la Mwenyezi Mungu aliyeumba viumbe vyote
b) Wakristo wanataka kuchinja kwa jina la nani?
c) Hii tabia ya kuchinja Waislamu imezoeleka tokea enzi za utawala wa mkoloni kama vile ilivyozoeleka kupumzika siku ya Jumapili.
d) Waislamu tuna ushahidi wa maandiko wa Mwenyezi Mungu kututaka tuchinje, sasa Wakristo wanataka kuchinja na andiko gani kwenye Biblia linalowaamrisha wachinje? Au wana nia ya kutaka kuwalisha watu vibudu?
Baada ya kumalizika kutolewa kwa hoja kwa pande zote mbili, Mkuu wa Mkoa Bwana Abbas Kandoro alisema jambo hilo la kuchinja serikali bado inalifanyia kazi, kwa sasa wenye haki ya kuchinja ni Waislamu.
Baada ya maneno hayo ya Kandoro alinyanyuka Mchungaji Mwamalupa na kumkabili kiongozi huyo wa serikali kwa maneno makali pasi na chembe ya woga.
Mchungaji huyo wa KKKT alimwambia huku akimkodolea macho Mkuu wa mkoa wa Mbeya kuwa yeye ni Muislamu, RPC Kamanda Diwani Athmani ni Muislamu na Afisa Uslama wa mkoa naye pia ni Muislamu, hivyo akadai wametoa maamuzi kwa kuwapendelea Waislamu wenziwao tu!
Kwa kweli kama binadamu, Mkuu huyo wa Mkoa alikwazika sana na kauli hiyo ambayo ilionekana kumshambulia yeye binafsi badala ya mamlaka aliyokwendanayo na kuwaita kwenye kikao hicho, lakini hakuchukua hatua yoyote hadi kikao kilipohairishwa.
Ilipofika Aprili 3, 2013 Wakristo wakapeleka Ng’ombe wao machinjioni huku kukiwa na ulinzi mkali wa jeshi la polisi kupita maelezo, mchinjaji ni Muislamu tena alikuwa akilindwa na askari polisi.
Kutokana na hali hiyo baadhi walikubali Ng’ombe wao kuendelea na kuchinjiwa na Waislamu, wengine waligoma na hivyo waliamua kurudi majumbani mwao wakiwa na mifugo yao.
Baada ya nyama kupelekwa mabuchani wale waliorudi na Ng’ombe wakaanzisha vurugu na kuwataka wenye mabucha kufunga mabucha yao ili kama ni kutopata fedha siku hiyo iwe kwa wote!
Wapo waliotii amri hiyo haramu ya Wakristo ambao walisalimika, lakini pia wapo waliogoma kutii ambao waliwatia hasira Wakristo na kuamua kutumia nguvu kuzifunga bucha hizo.
Kusikia hivyo polisi waliwahi na kuwatimua wachochezsi hao wa Kikristo ambapo baadae wakaona wakavamie misikiti ili watende jinai yao huko.
Walipobaini kuwa Waislam wameimarisha ulinzi katika misikiti yote iliyopo katika mji huo, kikundi hicho cha Wakristo kikaamua kuandamana hadi pembezoni kidogo mwa mji wa Tunduma ambako kuna msikiti mpya uliomalizika kujengwa na kuanza kuchoma moto huku wengine waking’oa madisha na milango na kutokomea kusikojulikana.
Lakini wakati wakiendelea na oparesheni yao hiyo ya kubomoa msikiti, polisi wakawa wameshapata habari na hivyo waliwasili eneo hilo na kufanikiwa kuwatia mbaroni watu 90 huku wengine wakikimbilia maporini.
Walipofikishwa katika kituo cha polisi baada ya mahojiano ikadaiwa 45 kati yao hawakuhusika na ghasia hizo ingawa wote walikamatwa kwenye eneo hilo,  hivyo wakaachiliwa!
Waliosalia yaani 45 ikaonekana ni lazima wafikishwe mahakamani na kwa kosa wanalotuhumiwa nalo na walisema hawatapatiwa dhamana.
Hata hivyo kikubwa kuliko yote ambacho Waislamu kuanzia wale wa Tunduma, Dar es Salaam na nchi nzima kwa ujumla wake kinachotushangaza ni kutokamatwa kwa Mchungaji Mwamalupa ambaye ndiye kinara wa chokochoko zote hizo.
Tunajiuliza hivi Mwamalupa angekuwa Imam, sheikh au hata Ustaadh angeendelea kuwa uraiani hadi leo? Kwanini jeshi la polisi mkoani Mbeya linamgwaya Mchungaji huyo?
KAULI YA OCD BAADA YA TUKIO
Katika hali ya kushangaza kamanda wa polisi wilayani Momba anawaambia waislamu kupitia kwa viongozi wao waliokwenda kuulizia sababu za watuhumiwa wao kuachiwa wote na kubaki saba tu!
 OCD aliwaambia wameachiwa kwa dhamana kwa kuwa dhamana ni haki ya kila mshitakiwa, pia akaongeza kusema kuwa, wanatakiwa wajitahidi kukusanya ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatihani washitakiwa hao, vinginevyo washitakiwa wote wataachiwa!
WASIWASI WETU KUHUSIANA NA KAULI YA OCD
Kwa kauli hii waislamu tunajiuliza, ni ushahidi gani unaotakiwa tuwasilishe mahakamani zaidi ya ule wa kubomolewa kwa msikiti ambao wenyewe polisi walishuhudia walipofika?
Lakini mbona katika kesi ya Waislamu polisi haiwaambii Wakristo waandae ushahidi wa kutosha vinginevyo Waislamu wote wataachiliwa?
Mbona waislamu wanaoshitakiwa kwa kesi ya kuchomwa makanisa Mbagala hatukusikia wakitakiwa Wchungaji kwenda kutoa ushahidi mahakamani? Iweje sisi tuambiwe tupeleke ushahidi wa kutosha hata kabla kesi haijasikilizwa? OCD huyu ana agenda gani nyuma ya kadhia hii?
Vurugu hizi za Tunduma tunaona ni mwendelezo uleule wa vurugu zilizowahi kutokea Busereser eMkoani Geita zilizosababishwa na maelekezo ya Maaskofu na Wachungaji wachache kwa waamini wao wa kujichinjia wanyama kwa ajili ya kitoweo na hata kuziuza mitaani.
(Rejea kauli ya Mkuu wa wilaya ya Geita Manzie Mangochie alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa gazeti la Mtanzania la Februar 11, 2013).
“Mchungaji wa FPCF katumia vipaza sauti kutangaza kuwa lazima wachinje na nyama kusambazwa kwenye bucha zao”, kufuatia tamko hilo Wakristo walichinja Ng’ombe na Mbuzi kwenye viwanja vya Kanisa lao na kusambaza katika bucha zilizopo katika soko la Msufini.
“Hili limetokea wapi? Naogopa sana wale wachache wanaopigania uchinjaji, mtu kama huyu anatia aibu Taifa letu. Inakuwaje Tanzania ya leo hawazungumzii tena matatizo tuliyokuwanayo na badala yake tunagombania uchinjaji hii ni aibu sana” hili ni tamko la Reginald Mengi kama alivyokaririwa na gazeti la Mwananchi la Aprli 9, 2013.
Ndugu zangu Waislamu, Shura ya Maimamu inaamini kwamba, suala hili la uchinjaji limeanzishwa kwa lengo la kuzuia serikali isizungumzie na kutafakari matatizo tuliyonayo ya uendeshaji wa nchi kwa MFUMO KRISTO! Hili liko wazi kabisa.
Aidha Shura ya Maimamu nchini Imepata faraja kusikia kwamba hata Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk Jakaya Kikwete anatambua tatizo la kuwanyima fursa Waislamu sambamba na fursa hizo kuwamiminia Wakristo kupitia MoU.
Hapa tutataja baadhi tu ya fursa wanazopata Wakristo kupitia mkataba huo kuwa ni pamoja na;-
   I.        Kutenga kiasi cha fedha za makusanyo ya kodi kwa ajili ya kuzipa asasi za afya na elimu zinazomilikiwa na Wakristo kwa ajili ya maendeleo yao.
II.        Kusaidia taasisi zinazomilikiwa na Makanisa kupata misaada kutoka kwa wafadhili wa nchi za nje.
III.        Kutenga nafasi maalum za masomo katika shule na vyuo kwa ajili ya kusomesha watakaofanya kazi katika taasisi za afya na elimu zinazomilikiwa na Makanisa.
IV.        Kuhakikisha kwamba serikali haitaifishi tena shule zinazomilikiwa na Makanisa pamoja na kuwa zinaendeshwa kupitia kodi za Watanzania.
KAMATAKAMATA YA MASHEIKH
Ndugu zangu Waislamu, tatizo jingine ambalo linakuwa kwa kasi ni kukamatwa kamatwa ovyo kwa viongozi wa Kiislamu pamoja na viongozi hao kunyimwa dhamana kwa kumtumia Mkurugenzi wa mashitaka (DPP) japo ni haki yao kwa mujibu wa sheria za nchi.
Inashangaza sana kuona jambo hili linatekelezwa sana pale wahusika wanapokuwa Waislamu.
Wakristo wao hawahusiki kabisa na sheria hiyo, mfano Machi 12, 2013 alikamatwa Katekista wa Kanisa Katoliki mkoani Simiyu kwa tuhuma za uchochezi pamoja na uvunjifu wa amani lakini mwisho wa siku aliachiwa kwa dhamana.
Siku hiyohiyo alikamatwa Mchungaji Christopher Mtikila mkoani Sumbawanga kwa kosa kama hilo la uchochezi, lakini naye pia aliachiliwa kwa dhamana!
Lakini alipokamatwa Imam Hamza Bin Omar Mwanza kwa kosa hilohilo la uchochezi amenyimwa dhamana hadi leo yuko ndani.
Halikadhalika Shekh Ponda Issa Ponda, sheikh Farid Had, Mselem Alli na wengineo wengi mpaka leo wako ndani baada ya kunyimwa dhamana. Je, hii ni haki kweli?
Tunafahamu kuwa mamlaka ya DPP kumnyima mtu dhamana yanaishia kwa afisa wa polisi na kwamba malaka hayo yapo chini ya hakimu au jaji.
Na ikiwa sheria inampa DPP mamlaka ya kuifunga mdomo mahakama kwa mnyima mshitakiwa dhamana, basi kusingekuwa na haja ya kuwepo mahakama.
Ndugu zangu, msikiti umevunjwa, mali na vifaa vingine vya msikiti yakiwemo  madirisha na milango vimeibiwa na hakuna kiongozi yeyote wa serikali aliyethubutu kupanua mdomo wake kulisemea hili achilia mbali kwenda kuwapa pole Waislamu wa Tunduma kama tulivyoshuhudia Wakristo wa Mbagala wakipewa pole!
Kwa mwenendo huu wa nchi kuongozwa ki-MFUMO KRISTO tutafika? Kwanini wale viongozi tuliowasikia wakilaani kuchomwa moto makanisa ya kule Mbagala leo wako kimya kulaani kubomolewa na kuchomwa moto msikiti wa Tunduma?
Ndugu zangu, imefika mahala hata baadhi ya Wakristo hususan wa kule Bukoba wamekuwa wakijiuliza, hivi haya yanayoendelea sasa hapa nchini ni suala la kuchinja tu ama kuna mkono wa siasa?
“Machi 13, 1978 pale Mwemage Parish kata ya Bwera tarafa ya Katerero mkoa wa Ziwa Magharibi enzi hizo (sasa Kagera) kulifanyika sherehe ya kuadhimisha miaka 25 ya Uaskofu wa Kadinal Lugambwa aliyesimikwa kuwa Askofu Mach 13, 1953.
“Katika hafla hiyo muhimu sana ya Kanisa jumla ya Ng’ombe watatu walichinjwa na waliohusika kuchinja walikuwa ni marehemu Mustafa Abdallah, sheikh Zahor Sinani na Mwalimu Said Salum Mutashobya ambaye zama hizo akiwa mwanajeshi wa JWTZ.
“Mutashobya bado yungali hai hadi leo na ni mwalimu wa madrasatil Swabiriin hapo Ibwera, mbali ya kuhusika katika uchinjaji pia ndiye aliyemlinda Askofu Lugambwa. Haya wanaweza kuyathibitisha Askofu Mstaafu Nestori Timanyisa wa Bukoba mjini na Askofu Mstaafu Gervas Nkaranga wa wa jimbo la Lulenge ambao walikuwepo siku hiyo, sasa leo ugomvi unatokea wapi?”, wanahoji Wakristo wa Bukoba.
Naye Mchungaji Anthony Lusekelo almaarufu ‘mzee wa upako’ wakati akiongea katika mojawapo ya vipindi vinavyorushwa na kituo cha televishen cha Channel 10 alisema anawashangaa kikundi kidogo cha Maaskofu wasiopenda amani ya nchi, wachochezi wenye tama ya kuiingiza nchi yetu katika machafuko, wao kama Wakristo hawana kibudu ila alisema wana haramu tu!
Akasisitiza kuwa, chochote kitakachochinjwa, iwe na Mkristo au Muislamu wao hawana tatizo nacho. Akasema anakumbuka sana enzi za udogo wake pale kwao Iringa kuku wote waliokuwa wakiandaliwa kwa ajili ya sherehe zao kuanzia ya PASAKA au KRISMAS walikuwa wakichinjiwa kwa sheikh Abdallah, sasa haya Maaskofu kung’ang’ania kuchinja yametoa wapi? Alihoji Lusekelo.
HITIMISHO;
Shura ya Maimamu inaitaka serikali iwachukulie hatua wale wote waliohusika na vurugu hizo na nguvu za dola ziwashukie
Tunaitaka serikali kukishughulikia kikundi cha viongozi wachache wa Kikristo wanaotoa maelekezo na maagizo kwa waumini wao kufanya vurugu za kuvunja misikiti na kusababisha uvunjifu wa amani ya nchi yetu.
Tunaitaka serikali kuweka utaratibu baina ya Wakristo na Waislamu kugawana Baraza la Mitihani (NECTA)  pamoja na fursa zinazopatikana katika MoU badala ya fursa hizo kupewa Wakristo peke yao.

0 comments:

Post a Comment