Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 9 April 2013

Sumatra: Ulevi unasababisha ajali kwa 76%

 MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) imebaini kuwa asilimia 76 ya ajali za barabarani zinasababishwa na matatizo ya kibinadamu, ukiwemo ulevi na uzembe wa madereva.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti walioufanya mwaka 2007 katika kutafuta chanzo cha ajali nyingi za barabarani ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.
Pamoja na matatizo hayo, pia utafiti huo ulibaini uchakavu na ubovu wa magari kuwa unachangia kwa asilimia 16 na ubovu wa barabara ni asilimia 8.
Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmed Kilima alitoa takwimu hizo wakati wa hafla fupi ya mamlaka hiyo kukabidhi kwa Jeshi la Polisi vifaa vya kupima ulevi kwa madereva 2,000 wa vyombo vya usafiri.
Alisema kuwa vifaa hivyo si vya muda mrefu, lakini wako mbioni kutafuta vya kudumu ili kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na ulevi.
Kilima alisema vifaa hivyo vitawasaidia kuwakamata madereva kabla ajali hazijatokea, kwani wengi wamekuwa wakinywa pombe kwenye chupa za maji na kusingizia kuwa ni maji.
Alisema kuwa vifaa hivyo vimegharimu sh milioni 12, lakini kwao hawajali gharama za ununuzi bali wanachotaka ni kuhakikisha Watanzania wako salama.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema alisema kuwa anaamini vifaa hivyo vitafanya vizuri katika kupunguza ajali za barabarani kama walivyofanya vizuri na kamera walizopewa na Sumatra miaka ya nyuma.
Alisema kuwa vifaa hivyo vimesaidia kujibu moja ya malengo ya Jeshi la Polisi ambalo ni kukinga ajali isitokee na vile vile kusaidia kudhibiti uhalifu.
IGP Mwema alisema kuwa katika kuhakikisha usalama barabarani jeshi hilo litashirikiana na Sumatra kuziwekea namba pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda, zitakazozitambulisha mikoa zinakotoa huduma kama ilivyo kwenye gari ndogo (teksi)

0 comments:

Post a Comment