Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 18 April 2013

Polisi yawahoji akina Kibamba


Ikiwa ni siku moja mara baada ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Deus Kibamba na Mratibu wa Jukwaa hilo, Diana Kidala, kudai kuwindwa na watu wasiojulikana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni limewahoji viongozi hao kwa takribani saa moja.
 
Akizumgumza na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kuwahoji viongozi hao, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema jeshi hilo liliwaita viongozi hao ili kupata ufafanuzi kwa mambo ya kiuchunguzi.
 
Kenyela alisema wamepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi hao na tayari polisi wameanza kuwasaka watu ambao wanadaiwa kuwawinda viongozi wa jukwaa hilo.
 
Aidha,Kenyela alisema watafanya uchunguzi wa kina ili kujua ukweli wa jambo hilo kwa kuwa kazi ya jeshi hilo ni kulinda usalama wa raia na mali zao.
 
Mapema wiki hii, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Jukwaa hilo, Hebron Mwakagenda, alisema watu walifika ofisi hapo majira ya saa sita mchana wakiwa na gari yenye namba za usajili T126 CCG ndipo walinzi wao wakawatilia mashaka watu hao baada ya kuwahoji wakadai viongozi hao ni marafiki zao.
 
Alisema cha kushangaza watu hao waliondoka katika mazingira ya kutatanisha bila kuaga au kuacha ujumbe wowote.

0 comments:

Post a Comment