Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 18 April 2013

Nundu ahoji Tanga kutokuwa na viwanda

MBUNGE wa Tanga Mjini, Omary Nundu (CCM), ameitaka serikali kueleza matayarisho inayoyafanya katika kufikia azima yake ya kuendeleza viwanda nchini na kurejesha Jiji la Tanga kuwa la viwanda kama ilivyokuwa kabla ya ubinafsishaji.
Nundu alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akiuliza swali ambapo alihoji kama azima hiyo inaweza kufikiwa kwa mwaka 2010-2015 na pia alitaka kujua hatima ya viwanda vya zamani vya sabuni ya Mbuni, Foma, Gadenia, Kiwanda cha Mashati cha Gossage na Kiwanda cha nguo cha CIC.
Pia alihoji hatima ya Kiwanda cha mbao cha Sikh, kiwanda cha chuma, Kiwanda cha Ambinin Plastics na kiwanda cha mbolea ambavyo vilimilikiwa na serikali na watu binafsi.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, alisema mkakati wa serikali kuufanya Mkoa wa Tanga kuwa jiji la viwanda upo katika hatua nzuri.
Alisema hivi sasa viwanda vilivyojengwa na vinavyojengwa ni pamoja na Kiwanda cha NILCANT cha kutengeneza chokaa, Kiwanda cha saruji cha Rhino Cement pamoja na Kiwanda cha saruji cha Sungura.
“Jiji la Tanga limeingia ubia na Kampuni ya Korea (GoodPM) kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kujenga viwanda 15 katika eneo la ekari 73 huko Pongwe unaotarajiwa kuanza Mei mwaka huu chini ya utaratibu wa Tanga Economic Corridor,” alisema Nagu.
Akizungumzia hatima ya viwanda vilivyokuwepo mkoani Tanga, Nagu alisema baadhi ya viwanda vinafanya kazi isipokuwa kiwanda cha chuma ambacho kimekarabatiwa na mazungumzo yanaendelea kati ya mwekezaji na CHC, ili kuanza kazi.
Pia alisema kiwanda cha mashati cha Gossage Kiwanda cha Gardenia na kile cha Amboni Plastic havifanyi kazi huku kiwanda cha mbolea kikiwa kimebadilishwa matumizi na sasa eneo hilo linatumika kama sehemu ya kuhifadhia mafuta.
Katika swali lake la nyongeza, Nundu aliitaka serikali kufanya tathmini na baadaye kuwapa wananchi wenye uwezo wa kuendeleza maeneo yaliyotelekezwa.
Akijibu swali hilo, Nagu alisema serikali italiangalia hilo na kueleza kuwa upo uwezekano wa kutoa maeneo ambayo wawekezaji wameyatelekeza ili wananchi waweze kuyaendeleza.
 

0 comments:

Post a Comment