Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 16 April 2013

Viongozi Jukwaa la Katiba wadai kuwindwa




 
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba nchini, Deus Kibamba na Mratibu wa Jukwaa hilo, Diana Kidala, wanawindwa na watu wasiofahamika na kina nia isiyoeleweka.

Jukwaa hilo limeeleza kwamba wiki iliyopita watu sita wakiwa kwenye gari aina ya Landcruiser walifika ofisini kwao wakiwatafuta kwa madai kwamba ni marafiki zao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa jukwaa hilo, Hebron Mwakagenda, alisema Aprili 6, mwaka huu watu hao walifika ofisini hapo majira ya saa sita mchana wakiwa na gari yenye namba za usajili T126 CCG ndipo walinzi wao wakawatilia mashaka baada ya kuwahoji wanashida gani wakadai viongozi hao ni marafiki zao.

Aidha,Mwakagenda alisema walinzi hao waliwatilia mashaka na kuwauliza watu hao kama viongozi hao marafiki zenu kwa nini msiwapigie simu au msiwafuate nyumbani kwao wakadai hawana namba zao za simu.  Alisema majibu hayo yaliwafanya walinzi wawatilie shaka na hivyo waliwakatalia.

Alisema baada ya watu hao kukataliwa kupewa namba za simu, walikaa nje ya geti kwa takribani saa moja na baadaye gari hiyo iliondoka na dereva pekee yake na watu sita waliokuwa ndani ya gari waliondoka  katika mazingira ya kutatanisha.

Aliongeza kuwa cha kushangaza watu hao waliondoka katika mazingira hayo bila kuaga au kuacha ujumbe wowote.

Alisema baada ya kikao cha mashauriano ndani ya Jukwaa waliamua kutoa taarifa hizo katika kituo cha polisi Mabatini na kufunguliwa jalada RB/KJN/RB2898/2013.

Alisema walimwandikia na kumjulisha Kamanda wa Polisi Kanda ya Kinondoni, Charles Kenyela, tukio zima lilivyokuwa huku wakiomba ofisi yake ianze uchunguzi.
Alisema nakala ya barua hiyo walimpelekea pia Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema.

Hata hivyo, alisema kwa kutambua jinsi nchi inavyoendelea kukumbwa na utekaji, utesaji na ukiukwaji wa haki za binadamu ndipo walipoamua kutoa tamko hilo kwa waandishi wa habari.

Mwakagenda alitumia fursa hiyo kuwaomba raia wote wema wawasaidie kutoa taarifa kwa jeshi la polisi wanapopata taarifa za njama zozote dhidi ya viongozi wakuu wa Jukwaa la Katiba.

Akizumgumzia tukio hilo, Kibamba alisema kutishiwa kwao hakutawarudisha nyuma katika utendaji wa kazi kwa kuwa wanafanyakazi kwa ajili ya wananchi.

Tukio hilo limetokea siku moja baada ya jukwaa hilo wiki iliyopita kuzungumza na waandishi wa habari jinsi mchakato mzima wa kupata mabaraza ya kata ulivyokuwa hauridhishi na kutishia kuiburuza tume ya Katiba Mahakamani.

0 comments:

Post a Comment