Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 11 April 2013

Mwinyi: Kila mtu ruksa kuchinja

 
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amerejea kauli yake kuhusu mgogoro wa udini akisema kila mtu ana haki ya kuchinja kutokana na imani yake ilimradi tu asivunje sheria za nchi.
Mwinyi alisema anashangaa kuona watu wakigombania kitu kidogo kama kuchinja ilihali Tanzania ina utamaduni wa amani siku zote na kwamba kila mtu ana imani yake ya dini anayoiamini.
Kiongozi huyo mstaafu alitoa msimamo huo jana jijini Dar es Salaam katika kongamano juu ya utamaduni wa Kiislamu Afrika Mashariki ambapo Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji.
“Imani ni nafsi ya mtu na haitakiwi kumlazimisha kula nyama iliyochinjwa na mwenzie. Na kama unaona aliyochinja mwenzio ni kibudu basi usile chinja yako, kula hata ukitaka kula chura, mjusi, konokono, kula utakacho ruksa ilimradi tu usiingie katika jinai,” alisema.
Mwinyi alikumbusha kuwa hata wakati wa utawala wake majaribu kama hayo yaliwahi kumtokea, lakini alijitahidi kuweka sawa kwa kumwambia kila mtu ale kile anachofikiri ni chakula bila kumlazimisha mwenzake.
Alisema Watanzania wamezaliwa ardhi moja na kwamba kinachotakiwa ni kuwa na misingi ya kuvumiliana, na kwamba sifa ya Uislamu ni pamoja na kuwa na uvumilivu.
Aliongeza kuwa Uislamu si kufanya vurugu kama inayotafsiriwa na makundi ya wanaotaka kuvunja amani ya nchi kwa kutumia jina la dini ya Kiislamu.
Pia alimshukuru Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ulimwengu wa Kiislamu Duniani (Rabita), Dk. Abdullah Mohsin Al-Turki kwa kuichagua Tanzania katika kuhubiri amani.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe ambaye alimuwakilisha Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilal katika kongamano hilo, alisema kuwa utamaduni wa Kiislamu Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla ni kuvumiliana katika dini.
Pia aliwataka Waislamu kujiendeleza katika elimu, akisema kuwa hata Mtume alihamasisha hayo, lakini Waislamu wameshindwa kuyafuata.
Prof. Maghembe alitoa mfano kuwa Waislamu wana Chuo Kikuu kimoja wakati dhehebu moja la Lutherani lina vyuo vikuu 11, akisema ni vyema wakaungana na kujenga vyuo kwa ajili ya kusaidia kuongeza wasomi katika taaluma mbalimbali.
“Suala la elimu ya dunia pia ni muhimu, lakini mfano mzuri wa elimu kushuka ni katika mikoa ya Pwani ambako ndiko ilipoanzia. Mathalani mwaka 1995 wanafunzi walioanza darasa la kwanza walikuwa 35,000 lakini waliomaliza darasa la saba ni 9,000. Hapa inaonesha Waislamu tunarudi nyuma,” alisema.
Akizungumza katika kongamano hilo, Dk. Abdullah Mohsin Al-Turki alisema katika nchi ya Saudia wanaishi watu tofauti, lakini wakiwa katika upendo huku akisisitiza kikubwa ni kuheshimiana.
Alisema Rabita imekuwa ikifanya kazi katika nchi mbalimbali za Nigeria, Gabon, Jamhuri ya Kongo na baada ya ziara yake nchini hapa atahitimisha kwa kuitembelea Sudan.
Kongamano hilo limeandaliwa na Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania likiwa na lengo la kusisitiza amani nchini.

0 comments:

Post a Comment