Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 25 April 2013

Mbunge akabidhi bungeni uthibitisho wa kauli yakeMbunge  wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), amekabidhi uthibitisho wa takwimu zinazoonyesha kuwa deni la Taifa linaongezeka kwa sababu matumizi ya serikali yanazidi mapato ya ndani.

Mpina aliwasilisha takwimu hizo jana baada ya kipindi cha mwaswali na majibu bungeni  kwa kurejea bajeti ya mwaka jana wa fedha ambapo alimuomba mwongozo Naibu Spika, Job Ndugai, aeleze kama majibu ya Naibu Waziri  wa Fedha, Saada Mkuya Salum, kwamba matumizi ya serikali hayazidi mapato ya ndani yanakidhi kanuni ya Bunge ya 46.

Kanuni ya 46 (1) inasema: “Waziri anayeulizwa swali atakuwa na wajibu wa kujibu swali hilo kwa ukamilifu kama alivyoulizwa, isipokuwa kama jibu linalohusika ni refu au lina takwimu nyingi, waziri atampa mbunge muuliza swali nakala ya jibu mapema baada ya kikao kuanza kabla ya muda wa kujibu swali hilo haujafikiwa.”

Alisema katika kipindi cha maswali na majibu, Aprili 16, mwaka huu, alipouliza swali la nyongeza lililohusu  deni la Taifa,  alisema moja ya sababu inayofanya deni la Taifa kuongezeka ni serikali kuwa na matumizi makubwa kuliko mapato ya ndani.

“Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, alisema hatukopi fedha kwa ajili ya matumizi ya ndani, tunakopa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo akanitaka nihakikishe kama takwimu zangu ziko sawa sawa. Nataka kukuhakikishia Mheshimiwa Naibu Spika kuwa takwimu zangu ni sahihi,” alisema.

Aliongeza: “Leo nimekuja na kitabu cha waziri cha bajeti ya mwaka 2012/2013 ambapo mapato yetu ya ndani yalikuwa Shilingi trilioni 9.1 wakati matumizi yetu ya kawaida yalikuwa Shilingi trilioni 10.6 kulikuwa na pungufu ya Shilingi trilioni 1.5.”

Alisema misaada iliyoipata nchi katika bajeti ya mwaka jana,  ilikuwa ni Sh. bilioni 878.4 na kwamba fedha zilizopungua katika bajeti hiyo zilifidiwa na fedha za kukopa.
Alisema kwa msingi huo matumizi ya serikali ni makubwa kuliko mapato ya ndani.

0 comments:

Post a Comment