Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 23 April 2013

Kinana: Tuache kutegemea wafadhili

                           

14Jumaadal Aakhir,1434 Hijiriyah/ April 24,2013 Miyladiyah
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdullahman Kinana, amewataka Watanzania kujenga misingi ya kujitegemea badala ya kuendelea kutegemea wahisani.
Kinana alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa, akihitimisha ziara yake ya siku nane mkoani Morogoro na kusema kuwa kwa muda mrefu, Watanzania wamesahau sera ya kujitegemea.
Alisema Tanzania itajengwa kwa kujitegemea, lakini sio kwa kuendelea kuwapigia magoti wafadhili.
“Tudumishe sera ya kujitegemea. Tukae imara tutengeneze mikakati ya kujitegemea,” alisema Kinana.
Akizungumzia hali ya kilimo katika mkoa huo, aliwapongeza baadhi ya vijana kwamba wengi wamejiajiri na wanafanya vizuri.
“Nimefika Ulanga nimeshangaa, wanajiajiri, hawasubiri serikali itoe ajira. Nimeshangazwa na jinsi wanavyolima kisasa, hongereni sana kwa kujitegemea,” alisema Kinana.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM, Kinana alimsifu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joe Bendera, kwa kusimamia utekelezaji huo.
Kwa mujibu wa Kinana, moja ya vipengele katika ilani za CCM ni kujenga daraja la Kilombero ambalo limeanza kujengwa na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.
“Kwa kasi hii ya utekelezaji wa ilani ya CCM, sina wasiwasi kabisa na uchaguzi mkuu ujao,” alisema Kinana na kuwaonya wana CCM wanaokiuka maadili kujiondoe wenyewe.
Kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaoendelea, Kinana alikitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutojitoa kwani Katiba hiyo ni mali ya Watanzania wote na sio CCM.
Alisema haoni sababu ya msingi ya CHADEMA kutishia kujitoa, kwani tume iliyoundwa ina watu makini na inafanya kazi kwa weledi.

0 comments:

Post a Comment