Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 30 April 2013

Kigonda awakingia kifua wamachinga

 
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, ameeleza kushangazwa na hatua ya wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga kufukuzwa katika maeneo wanayofanyia biashara ambapo katika nchi nyingine duniani wamekuwa wakienziwa.
Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na ITV, Dk. Kigoda alisema kama waziri mwenye dhamana, anashangazwa na hali hiyo na kwamba kuna haja kwake kukaa na halmashauri kuona namna ya kushughulikia tatizo hilo.
“Mimi kitu kimoja kinachinishangaza na si kunishangaza tu, nimetembea nchi nyingi sana duniani, na hawa wafanyabiashara wadogo wadogo wapo kila mahali, ukienda Uchina utawakuta, Thailand utawakuta, Morocco, Afrika Kusini utawakuta, lakini wanafanya kazi zao tu.
“Lakini sisi hapa hapana, ndiyo maana nasema labda tunapambana na tatizo na si chanzo cha tatizo, utakuta wanafukuzwa, wanaondolewa lakini katika maeneo mengine wanafanya kazi zao vizuri, sisi hapa kwa nini tunakuwa tofauti?” alihoji.
Alisisitiza kuwa anataka kujaribu kurekebisha suala hilo kwani anadhani kuwa hata wafanyabiashara hao ambao wamekuwa wakifanya kazi zao kihalali ili kujitafutia kipato hawapendi kufukuzwa.
Waziri Kigoda aliongeza kuwa ukienda nchi za nje utakuta wafanyabiashara ndogo ndogo wakifanya biashara zao katika maeneo yao bila kusukumwa, hivyo kuna haja kwa elimu kubwa kutolewa hapa nchini kama njia ya kuwasaidia ili waweze kufanya kazi katika maeneo mazuri.
Alitolea mfano Soko la Machinga Complex na kuhoji namna linavyotumika kwani kwenye nchi kama Morocco kuna sehemu ukitaka kitu fulani utaambiwa uende sehemu fulani lakini iweje hapa nchini.
Alisema kuna haja ya kutafuta ufumbuzi wa suala hilo ili wafanyabiashara hao wafanye kazi bila kuingiliwa.
Alisema anaamini hoja yake ya kukaa na halmashauri itasaidia kulitafutia ufumbuzi suala hilo kuliko kuwafanyia vinginevyo kwani wafanyabiashara waliopo ni wengi na wamekuwa wakifanya shughuli zao kama sehemu ya kujipatia ajira.

0 comments:

Post a Comment