Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 18 April 2013

Kesi saba za ufisadi kukamilika mwaka huu

Serikali imesema kuwa uchunguzi wa tuhuma kubwa saba za ufisadi utakamilika katika mwaka wa fedha 2013/14.

Jukumu hilo litatekelezwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).

Hatua hiyo ilitangazwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, wakati akiwasilisha makadirio ya ofisi hiyo mwaka mwaka 2014/14.

“Takukuru imepanga kukamilisha uchunguzi wa tuhuma saba za rushwa kubwa kama ilivyopangwa katika Mpango Mkakati wa Taasisi,” alisema Kombani.

Aliongeza kwamba vile vile, Takukuru itaendelea kuendesha kesi 495 zilizoko mahakamani na zitakazoendelea kufunguliwa kutokana na kukamilika kwa uchunguzi mbalimbali.

Hata hivyo, Kombani hakuzitaja tuhuma hizo saba kubwa za rushwa ambazo uchunguzi wake utakamilishwa na Takukuru.

Licha ya Kombani kutokuzitaja tuhuma hizo za ufisadi, lakini kumekuwapo na tuhuma kadhaa ambazo zimekuwa zikitajwa na Takukuru kueleza kuwa uchunguzi wake unaendelea.

Baadhi ya tuhuma hizo kubwa za ufisadi ni kuhusu kampuni hewa ya Kagoda Agriculture Ltd ambayo ilichota Sh. bilioni 40 kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kagoda ambayo wamiliki wake hadi leo hawajafahamika ilichote fedha hizo mwaka 2005 kati ya Sh. bilioni 133 zilizochotwa BoT ikidai kuwa zilichukuliwa kwa ajili ya masuala ya usalama.
Tuhuma nyingine ni kuhusu kashfa ya ununuzi wa rada iliyonunuliwa na serikali mapema miaka ya 2000 kutoka Uingereza kwa bei ya juu kuliko thamani yake halisi.

Mwaka 2011, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari jijini Arusha, kuwa taasisi hiyo ilikuwa inaendelea kuchunguza Kagoda na kashfa ya rada.

Tuhuma nyingine ambazo zinaendelea kuchunguza ni zinazomhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, za kuchangisha fedha kutoka taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo kwa lengo la kuwashawishi waabunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2011/12.

Tuhuma nyingine zinazochunguzwa na Takukuru ni dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Blandina Nyoni, anayetuhumiwa kwa tuhuma kadhaa ambazo zilisababisha mgomo wa madaktari nchini.

Tuhuma nyingine za ufisadi ambazo zimekuwa zikitajwa zinahusu Kampuni ya Meremeta, Tangold, Deep Green na nyingine ambazo ziliisababishia serikali kupoteza mabilioni ya Shilingi.
 

0 comments:

Post a Comment