Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 23 April 2013

Kasoro kwenye notisi zakwamisha rufaa ya Zombe


Mahakama ya Rufaa Tanzania jana ilishindwa kusikiliza ombi la rufaa dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Abdallah Zombe na wenzake wanane kutokana na kasoro katika notisi ya rufaa.

Notisi hiyo iliwasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akionyesha nia ya kukata rufaa kwenye mahakama hiyo.

Kasoro zilizojitokeza kwenye notisi ya rufaa ni kumtaja Jaji Salum Massati kama Jaji wa Mahakama ya Rufaa wakati kesi ikiwa katika mahakama hiyo hiyo kuitaka itoe maamuzi.

Maombi hayo yaliletwa mbele ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, wakiongozwa Jaji Edward Rutakankwa, Mbaruku Salum Mbaruku na Bethueri Mmila.

Kikatiba Mahakama ya Rufaa haiwezi kutoa maamuzi yalitotolewa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Awali, wakati Jaji Massati anaendelea na usikilizaji wa kesi ya msingi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, na kwenye notisi hiyo wamemtaja kama Jaji wa Mahakama ya Rufaa ambayo rufaa imewasilishwa.

Kutokana na hali hiyo, Wakili wa utetezi, Majura Magafu, aliiomba Mahakama hiyo kutupilia mbali ombi la kukata rufaa kutokana na kasoro zilizojitokeza.

“Notisi ya rufaa ndiyo inatengeneza rufaa, kama notisi inakasoro basi hata rufaa haitakuwa sahihi, tunaiomba mahakama itupilie mbali,” alidai Wakili huyo.

Awali, kabla ya Wakili huyo kuwasilisha ombi hilo, Mahakama hiyo ilieleza kuona kasoro hizo.
Wakili Mkuu wa Serikali, Vitalis Timon, alikiri kuwepo kwa kasoro hizo na kudai kuwa zipo kwenye notisi lakini rufaa imeandikwa cheo chake kwa ufasaha.

Aidha, aliiomba mahakama hiyo kuwapa muda kwa ajili ya kufanya marebisho ya kasoro hizo na kuiwasilisha mahakamani hapo.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, mahakama hiyo ilisema itatoa tarehe ya uamuzi kama upande wa mashtaka upewe nafasi ya kufanya marekebisho au la.

Kwa mara ya kwanza, Afande Zombe alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu, akituhumiwa kwa mauaji ya watu wannne; Ephraim Sabinus Chigumbi, Sabinus Chigumbi Jongo, Juma Ngugu na Mathias Lunkombe.

Katika kesi hiyo, Zombe na wenzake hao walikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese, Dar es Salaam.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa walikuwa ni Zombe, ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Noel Leonard, Konstebo Jane Andrew, Koplo Nyangerela Moris, Konstebo Emmanuel Mabula na Koplo Felix Sedrick,

Wengine walikuwa ni Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Koplo Rashid Lema (aliyefariki kabla ya kujitetea), Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.

Washtakiwa hao walikuwa wakidaiwa kuwa Januari 14, 2006, katika Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam, waliwaua kwa makusudi wafanyabiashara waliokwenda kuuza madini yao Dar es Salaam na dereva teksi aliyekuwa akiwaendesha.

Katika hukumu ya Jaji Massati aliagiza upande wa Jamhuri kuwasaka na kuwakamata wauaji waliohusika na mauaji ya wafanyabiashara.

Oktoba 06, 2009, DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu.
Katika rufani hiyo DPP alidai kuwa Jaji Massati aliyetoa hukumu hiyo, alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao kwani kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.


0 comments:

Post a Comment