Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday 21 April 2013

Ikulu yamkana Rais wa CWT

                        11Jumaadal Aakhir,1434 Hijiriyah/ April 21,2013 Miyladiyah 

SERIKALI imesema kauli iliyotolewa na Rais wa Chama cha Walimu nchini (CWT), Gratian Mukoba kwenye vyombo vya habari kuwa imekataa kukaa meza moja na walimu haina ukweli hata chembe.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema kuwa madai hayo hayana nia njema, maana yanaweza kujenga chuki na mazingira ya kuzua mgogoro mwingine na serikali usio na sababu wala maslahi kwa walimu wenyewe na taifa.
Kwa mujibu wa Ikulu, serikali haijakataa majadiliano na CWT, na wala haijapuuza amri ya mahakama inayotaka pande zote mbili kurudi kwenye meza ya majadiliano.
“Tangu amri ya mahakama itolewe, tayari vimefanyika vikao vinne vya Baraza la Majadiliano ya pamoja katika utumishi wa walimu. Vikao viwili vilifanyika mwaka jana Septemba 12 na Desemba 5. Vikao viwili tayari vimefanyika mwaka huu Januari 9 hadi 10 na Machi 22,” ilisomeka taarifa hiyo.
Iliongeza kuwa kilichochelewesha suala la mishahara na posho kujadiliwa katika vikao hivyo si kwamba serikali haikutaka mjadala huo, bali CWT ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, katika kesi Na. 96/2012.
Kwamba japo serikali iliwasihi sana viongozi wa CWT wafute rufaa hiyo ili kuruhusu majadiliano ya mishahara na posho, lakini walikataa. Kitendo hicho hakionyeshi nia njema upande wao.
“Sababu ya pili iliyochelewesha majadiliano ya maslahi ya walimu ni madai ambayo awali viongozi wa CWT walikuja nayo kuwa iteuliwe timu maalumu ya kuzungumzia maslahi badala ya Baraza la Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Walimu ambalo ndilo lipo kisheria kwa majadiliano haya.
“Ni kwenye kikao cha Januari 9-10 mwaka huu ndipo walipokubali kurejesha majadiliano kwenye baraza hilo. Si kweli vile vile kuwa kikao kilichofanyika Ikulu, Aprili 2 mwaka jana, chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ndicho kilikataa majadiliano kuhusu maslahi ya walimu,” ilisema.
Ikulu ilifafanua kuwa mkutano wa Aprili 2 mwaka huu, uliitishwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa maombi rasmi ya uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) ambao walitaka kujulishwa jinsi utaratibu wa majadiliano ya mishahara ya wafanyakazi wote utakavyokuwa kufuatia kuanzishwa kwa mzunguko mpya wa bajeti ya serikali.
“Tunapenda wananchi na walimu wajue pia kuwa Mukoba hakuwepo kwenye hicho kikao cha Aprili 2, 2013. Aidha, kikao hicho kilikuwa cha TUCTA, hakikuwa cha CWT,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Kauli ya Ikulu imekuja baada ya Mukoba kukaririwa na vyombo vya habari Aprili 9 mwaka huu, akisema kuwa serikali inakaribisha mgogoro mwingine kutokana na kukataa kukaa meza moja na CWT ili kuzungumzia nyongeza ya mishahara na posho za walimu.

0 comments:

Post a Comment