Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday, 21 April 2013

DR.SHEIN: MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA ZISHIRIKIANE KUPAMBANA NA WIZI ZNZ

                          11Jumaadal Aakhir,1434 Hijiriyah/ April 21,2013 Miyladiyah 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amezitaka mamlaka za mikoa na serikali za mitaa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti wimbi la wizi wa mazao na mifugo lililoshika kasi Zanzibar hivi sasa.
Alisema suala hilo lazima lishughulikiwe vizuri na kwa umakini mkubwa kwa sababu hatua iliyofikiwa sasa na vitendo vya baadhi ya wezi kukata sehemu za viungo vya mifugo kama ng’ombe na kuwaacha wazima sio tu kuwa ni ukatili bali pia haviwezi kufikiriwa kufanywa Zanzibar.
Dk. Shein alitoa wito huo wakati akihitimisha majadiliano ya mkutano wa tathmini ya taarifa ya utekelezaji mpango kazi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Idara ya Uratibu Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa uliofanyika jana Ikulu.
“Ni vitendo vibaya na vya kikatili kukata baadhi ya viungo vya mnyama bila kuchinjwa huku ukimwacha akihangaika kwa maumivu. Lazima tuwe makini na hatua za kuchukua kwa kuwa wanaofanya vitendo hivi si watu wa kawaida,” alisema.
Alisema hofu yake ni kuwa nyama hiyo huishia kuuzwa kwa matumizi mbalimbali ya wananchi kitendo ambacho kinaingilia hata imani ya dini.
Sambamba na agizo hilo, Dk. Shein aliwakumbusha viongozi na watendaji wa mamlaka hizo kuelewa kuwa ndizo zilizo karibu na jamii hivyo kila wakati wawe tayari kupokea na kutafuta njia za kukabiliana na changamoto.
“Huko mliko ndiko kwenye wananchi… sisi wote humu (kikaoni) tunaishi katika maeneo ya mamlaka zenu, hivyo hoja zitakuja, malalamiko yatakuja na hata pongezi wakati mwingine wananchi watakuja nazo, zote tuzipokee,” alisema.

0 comments:

Post a Comment