Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 23 April 2013

Dk. Hoseah: Rushwa imetuvunjia heshima

                          
 
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), imekiri kwamba tatizo la rushwa nchini ni kubwa na sasa limeivunjia heshima Tanzania katika macho ya jamii ya kimataifa.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu mapambano dhidi ya rushwa kwa viongozi wa madhehebu ya dini kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Alisema Tanzania ilikuwa ikiheshimika katika jamii ya kimataifa, lakini tatizo la rushwa limeiondolea heshima kwani limesababisha kukosa amani.
Dk. Hoseah alisema rushwa ni dhambi na kuwataka viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kutafakari uzito wa tatizo hilo hapa nchini na kwamba vita dhidi yake ipewe kipaumbele kama ilivyo kwenye kampeni ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Alisema tatizo linalokwaza taasisi yake katika mapambano dhidi ya rushwa ni ukubwa wa nchi pamoja na kuwa na watumishi wachache ambao hushindwa kuyafikia maeneo mengi kwa uharaka.
Akizungumza na waandishi baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Dk. Hoseah alisema kuwa rushwa ni matumizi mabaya ya madaraka yanayowanyima wananchi haki zao za msingi.
Kwa mujibu wa Dk. Hoseah, nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zinapoteza kiasi cha dola bilioni 276 kila mwaka, hiyo ikiwa ni ripoti ya Global Financial Integrity (GFI) ya mwaka 2000-2009.
Alifafanua kuwa agenda ya taasisi yake kwa sasa ni ushirikiano na si kuanza kulaumiana.
Kuhusu tatizo la ucheleweshwaji wa kesi zinazohusiana na rushwa, Dk. Hoseah aliahidi kulitafutia ufumbuzi wa kina na haraka.
Alisema taasisi yake inaweka mikakati wa kukutana na Jaji Mkuu kwa ajili ya kufanya mazungumzo na kuangalia tatizo la ucheleweshwaji wa kesi zinazohusiana na uchaguzi pamoja na nyinginezo.
Kuhusu ukubwa wa tatizo la rushwa katika nchi za Afrika Mashariki, Dk. Hoseah alisema Rwanda inachukua nafasi ya kwanza katika kukabiliana rushwa ikifuatiwa na Tanzania, huku Kenya ikishika nafasi ya tatu ikifuatiwa na Uganda

0 comments:

Post a Comment