Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 9 April 2013

China yahamasishwa kuwekeza kwenye utalii

TANZANIA imewahamasisha wawekezaji kutoka China kuwekeza katika sekta ya utalii ambayo ina fursa nyingi ambazo bado hazijatumiwa ipasavyo.
Mkurugenzi wa Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ibrahim Mussa alisema hayo jana alipokutana na ujumbe wa Kamisheni ya Utalii ya Chaoyang jijini Beijing nchini China.
Mussa ambaye anaongoza ujumbe kutoka Tanzania unaotembelea China kwa lengo la kutangaza utalii, alisema kuwa wana matarajio makubwa ya kupata wawekezaji kutoka China hasa katika maeneo ya uwekezaji wa hoteli ili kuongeza idadi ya vitanda nchini.
Alisema hatua hiyo inalenga kukidhi mahitaji ya watalii wanaofika nchini kutalii. Pia utaalamu wa mafunzo kwa ajili ya rasilimali watu katika sekta ya utalii inahitajika ili kuweza kuhudumia watalii wanaofika nchini katika viwango vinavyokubalika kimataifa na hivyo kuwataka Wachina kutumia fursa hizo kuisadia Tanzania.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allan Kijazi alisema kuwa wameshaandaa mwongozo kwa wawekezaji unaobainisha fursa mbalimbali za uwekezaji katika hifadhi hizo.
Alisema kuwa mwongozo huo hivi sasa umetenga maeneo 25 kwa ajili ya uwekezaji ikiwemo manne katika Hifadhi ya Serengeti; matatu katika Hifadhi ya Tarangire, sita Hifadhi ya Katavi na manne Hifadhi ya Saadani.
Kwamba wawekezaji wanahimizwa kuwekeza wakiwemo wa kutoka China ambayo ukuaji wake kiuchumi unakwenda kwa kasi kubwa.
Kijazi aliongeza kuwa hivi sasa wawekezaji katika maeneo ya hifadhi wanatoka katika mataifa ya Marekani na Ulaya na kwamba hakuna wawekezaji kutoka China na hivyo kuwahimiza sasa kutumia fursa zilizopo katika hifadhi kwa ajili ya kuwekeza.
Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii nchini, Dk. Aloyce Nzuki alihimiza mashirika ya kuratibu safari za wageni yanayomilikiwa na serikali nchini China kufungua matawi ya ofisi zao nchini ili kusaidia kuongeza idadi ya wageni kutembelea vivutio vya utalii.
 

0 comments:

Post a Comment