Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 11 April 2013

Chakua yairuka Sumatra

SIKU moja kabla ya kuanza kutumika kwa nauli mpya za daladala na mabasi yaendayo mikoani, Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA) kimesema hakijakubaliana na Mamlaka ya Kudhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kupandisha nauli hizo.
Chama hicho kimetoa kauli hiyo baada ya maofisa wa Sumatra kudai kushirikisha chama hicho katika kikao chao cha mwisho cha kujadili kupanda kwa nauli kabla ya kutoa tangazo Aprili 2, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Hassan Mchanjama alisema kitendo walichokifanya Sumatra ni cha upotoshaji, kwani kinasababisha jamii kutoona umuhimu wa chama chao kutokana na kutotetea abiria kama kilivyosajiliwa.
“Mara ya mwisho kukutana na Sumatra ni kwenye kikao cha kujadili nauli za treni za Mwakyembe, nashangaa wamekutana na sisi wapi tena? Kisheria wanatuma barua, kama wanazo waje wathibitishe kama wametualika,” alisema.
Mchanjama alisema walishawahi kushauri Sumatra kurekebisha huduma za usafiri kabla ya kupandisha nauli, lakini hawakufanya hivyo badala yake wamekutana na wamiliki na kuamua kupandisha nauli.
Aidha, alisema kupanda nauli, kwa abiria wa mikoani ni kuwaongezea mzigo kwani wamekuwa wakiteseka kwa kulipa nauli ya abiria na mizigo yao.
Mkurugenzi wa chama hicho, Tomas Haule alisema wameshatuma barua kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe mwanzoni mwa wiki hii ya kuomba kusitishwa upandishaji wa nauli hizo.

0 comments:

Post a Comment