Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 11 April 2013

CAG aibua madudu mapya

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  Bw Ludovick S. L. Utouh
--
WIZARA ya Nishati na Madini imekumbwa na kashfa mpya ya kushindwa kukusanya kiasi cha dola 12,634,354, sawa na sh bilioni 19.7 kama sehemu ya mirabaha kutoka kwenye kampuni zinazochimba madini nchini.
Mbali na kushindwa kukusanya kiasi hicho cha mirabaha, pia imeshindwa kukusanya kiasi cha sh 1,645,582,899 kutoka vyanzo mbalimbali kama vile vitalu vya madini na leseni za umeme.
Hayo yamebainika katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2012, iliyowasilishwa bungeni jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Utouh alisema kuwa maduhuli yaliyoshindwa kukusanywa na wizara hiyo yalitokana na mabadiliko ya sheria ya madini iliyorekebisha kiwango cha mrabaha kutoka asilimia 3 hadi 4.
Mbali ya Nishati na Madini, wizara nyingine iliyokumbwa na madudu ni ya Ujenzi, ambayo kwa mujibu wa ripoti ya CAG, iliamua kutumia sh milioni 252.9 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya ujenzi wa barabara na badala yake ililipia madeni yanayowakabili.
Upungufu mwingine uliobainishwa katika ripoti hiyo ni pamoja na kuongezeka kwa fedha za misamaha ya kodi, ambapo katika kipindi hicho, serikali ilitoa misamaha ya kodi ya sh trilioni 1.9 kutoka trilioni moja, sawa na ongezeko la asilimia 27 kutoka 18.
Alisema kuanzia mwaka ujao wa fedha, ofisi yake itakagua misamaha yote ya kodi inayotolewa na serikali na kuwatangaza hadharani makampuni, mashirika, wafanyabiashara na watu binafsi wanaopata misamaha ya kodi.
Akizungumzia upungufu uliojitokeza kwenye ukaguzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Utouh alisema kwamba kumekuwa na udhaifu mkubwa katika kusimamia mapato ya ndani.
Alitaja upungufu huo kuwa ni vitabu 2,990 vya stakabadhi za mapato kutoka halmashauri 36 kutokutolewa kwa ajili ya ukaguzi wakati halmashauri 56 zilikuwa na jumla ya sh bilioni 4.4, ikiwa ni mapato yaliyokusanywa na mawakala ambao hawajawasilisha kwenye halmashauri hizo.
“Halmashauri 17 hazikukusanya kodi ya majengo kiasi cha sh bilioni 4.3, sawa na asilimia 38,” alisema.
Kama ilivyokuwa katika taarifa yake ya mwaka jana, ukaguzi wa mwaka huu pia umebaini kuwapo kwa watumishi 17,710 ambao wamekuwa wakipokea mishahara pungufu, 1/3 ya mishahara yao, kinyume cha sheria kutokana na watumishi hao kuelemewa na mikopo.
Pia ripoti hiyo imeendelea kubaini kuwa kuna watumishi hewa, wakiwamo waliostaafu na waliofariki dunia, wameendelea kulipwa mishahara ya sh milioni 82.3.
Akizungumzia Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali Kuu, CAG alisema mfuko huo una hali mbaya, kwani hadi sasa una hasara ya sh trilioni 6.4, hivyo kuwa kwenye hatari ya kufa.
Hata hivyo alisema pamoja na mfuko huo kuwa na hali mbaya kifedha, amebaini kuwa ulitoa mikopo ya sh bilioni 67 kwa taasisi za umma na nyingine bila riba na mikopo hiyo ilidhaminiwa na serikali.
Alizitaja taasisi zinazodaiwa na kiasi cha fedha kwenye mabano kuwa ni pamoja na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) sh bilioni 54.6, PCCB (sh bilioni 6.6), Tan Power Resources (sh bilioni 5.4) na Kiwanda cha Madawa Tanzania (sh milioni 485).
Hata hivyo alisema matokeo ya ripoti ya mwaka huu, yameonesha kuboreka kwa hati zilizotolewa kwa Serikali Kuu na taasisi zake ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Alisema hati za kuridhisha zimeongezeka kutoka 69 mwaka 2011/2011 hadi 108 wakati hati zenye shaka zimepungua kutoka 12 hadi sita mwaka 2011/2012 na hapakuwa na hati isiyoridhisha wala hati mbaya  kama ilivyokuwa mwaka 2010/2011.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (POAC), Zitto Kabwe, alisema pamoja na mabadilko machache, bado ripoti hiyo ni mbaya, kwani bado kuna matatizo makubwa ya usimamizi wa fedha za serikali.
Alishangaa Wizara ya Nishati na Madini kushindwa kukusanya mirabaha kutoka makampuni ya madini na kusisitiza kwamba kuna kazi kubwa ya kuibana serikali katika kusimamia matumizi ya fedha za umma.
 
 

0 comments:

Post a Comment