Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 30 April 2013

11 wachukua fomu CUF

 
WANACHAMA 11 wa Chama cha Wananchi (CUF) wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea ubunge katika Jimbo la Chambani, lililoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Salim Hemed Khamis, aliyefariki dunia hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo, mkutano wa Baraza Kuu wa kuchuja mgombea utafanyika Mei 12 na 13 mwaka huu chini ya Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba.
“Tayari Kamati tendaji taifa inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Katibu Mkuu wa chama, Maalim Seif Sharrif Hamad, imeshawapa wajumbe wote taarifa za kikao hicho, hivyo tuko katika maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kikao,” alisema.
Mketo aliongeza kuwa mara baada ya kikao hicho, wataandaa bajeti kwa ajili ya kulivamia jimbo hilo katika kampeni ambazo alidai kuwa zitakuwa za nguvu kwa kuwa wamejipanga kulirejesha.
Mbali na CUF vyama vingine ambavyo vimetangaza kusimamisha wagombea ni CHADEMA na CCM.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema chama chao kipo katika maandalizi ya awali katika uchaguzi mdogo wa Chambani na kata 26 ambazo zipo wazi.
Pia Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kwamba utaratibu wa kumpata mgombea mmoja ambaye atachuana na vyama vingine umeanza kwa kufanyika vikao katika eneo, kata/jimbo husika na kuendelea mpaka taifa.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika Juni 16, mwaka huu, ambapo kampeni zinatakiwa kuanza Mei 18 hadi Juni 15, mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment